
Ofisi ya Mchunguzi wa Vifo ya Kaunti ya Los Angeles, Marekani imethibitisha kuwa idadi ya vifo vilivyotokana na moto wa msituni unaoteketeza maeneo ya jiji la Los Angeles imeongezeka na kufikia watu 16.
Taarifa iliyotolewa Jumamosi jioni, Jan 11 2025, imeeleza kuwa vifo vitano vimetokana na Moto wa Palisades, huku vifo vingine 11 vikihusishwa na Moto wa Eaton. Hadi sasa, matukio haya bado yanaendelea kuchunguzwa. Awali, idadi ya vifo vilivyothibitishwa ilikuwa 11, lakini maafisa walionya kuwa idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka kadri mbwa wa kunusa wanavyoendelea kutafuta miili kwenye maeneo yaliyoathiriwa, na vikosi vya uokoaji vikiendelea kutathmini uharibifu.
Mamlaka zimeanzisha kituo maalum kwa ajili ya watu kuripoti ndugu au jamaa waliopotea.
Wakati huo huo, Jeshi la Zimamoto linakimbizana na muda kujaribu kudhibiti moto kabla ya upepo mkali unaotarajiwa kuanza, ambao unaweza kusababisha moto kusambaa kuelekea kwenye maeneo ya makumbusho kama kwenye Jumba la Makumbusho la J. Paul Getty na Chuo Kikuu cha California, Los Angeles.
Tahadhari mpya za kuhamisha watu zimetolewa, jambo lililoongeza wasiwasi miongoni mwa wakazi.
Mapambano makali dhidi ya moto yanaendelea katika maeneo ya Mandeville Canyon, eneo linalojulikana kwa kuwa makazi ya watu mashuhuri kama Arnold Schwarzenegger, karibu na Pwani ya Pasifiki. Helikopta zimekuwa zikiruka juu ya maeneo yaliyoathirika, zikimwaga maji kwenye moto unaoelekea milimani.
Zimamoto waliokuwa ardhini walitumia mabomba ya maji kupambana na moto unaoruka huku moshi mzito ukifunika vilima vilivyofunikwa na mimea mikavu.
Moto huu umeendelea kusababisha hofu na uharibifu mkubwa katika maeneo mengi ya Kaunti ya Los Angeles. Endelea kufuatiulia.