×

Kiboko Aliyetesa Wananchi Kwa Miaka Mitano Auawa Na Askari Wa Wanyamapori Geita – Video

BAADA ya kiboko kuua ng’ombe watatu na kuharibu mazao ya mahindi katika kijiji cha Itale, Kata ya Katoma, Halmashauri ya Wilaya ya Geita, mnyama huyo hatimaye amedhibitiwa na askari wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA).

Kwa mujibu wa Mwakilishi wa Kamanda wa Uhifadhi wa TAWA, Kanda ya Ziwa, Afisa Wanyamapori Msaidizi Daraja la Pili, Sefu Marambo, hatua hiyo imefuatia barua ya wito iliyotumwa kutoka Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Geita. Amesema kikosi cha TAWA kilifika kijijini hapo mara moja na kufanikisha kumdhibiti mnyama huyo.

Kamanda wa Uhifadhi wa TAWA, Kanda ya Ziwa, Afisa Wanyamapori Msaidizi Daraja la Pili, Sefu Marambo

Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Itale, Michael Gongoro, amesema kuwa wakazi wa kijiji sasa wamepata amani baada ya kiboko huyo kuhatarisha usalama wa watu, mifugo, na mazao kwa zaidi ya miaka mitano.

Wananchi wa kijiji hicho wametoa shukrani zao kwa TAWA kwa kutatua changamoto hiyo. Kiboko huyo, anayekadiriwa kuwa na uzito wa tani tano (kilo 5,000), ameua ng’ombe watatu na kujeruhi wengine mwaka huu pekee. Baada ya kumuua kiboko huyo wananchi wamepewa nyama yake kama kitoweo.

Leave a Comment