×

Cecot: Gereza La Kutisha La Wafungwa Wa Magenge Hatari, Hawaoni Jua, Kutoroka Haiwezekaniki Kabisa – Video


Nchi ya El Salvador, iliyoko katika bara la Amerika ya Kati, imechukua moja ya hatua kali zaidi katika vita vyake dhidi ya magenge ya uhalifu kwa kujenga gereza walioliita Kituo cha Kuzuilia Magaidi, au kwa kifupi CECOT.

Gereza hili kubwa zaidi kuwahi kujengwa Amerika ya Kusini na dunia nzima, lililoundwa kuhifadhi wahalifu hatari zaidi wa nchi hiyo, limekuwa ishara ya msimamo mkali wa Rais Nayib Bukele dhidi ya uhalifu. Lakini kadiri kituo hiki kinavyozidi kujaa, maswali yanaibuka kuhusu ufanisi wake wa muda mrefu na masuala ya haki za binadamu yanayohusiana nacho.

Likiwa katika eneo la Tecoluca, San Vicente, CECOT ndilo gereza kubwa zaidi na lenye ulinzi mkali zaidi Amerika ya Kati. Lilijengwa kwa muda wa miezi saba tu kwa gharama ya dola za kimarekani milioni 100 na linachukua eneo la ekari 410, likiwa na uwezo wa kuwahifadhi wafungwa 40,000.

Lilitengenezwa mahsusi kuwazuia wanachama wa magenge hatari ya uhalifu ya kundi la MS-13 na Barrio 18—makundi ya uhalifu yaliyoitesa El Salvador kwa miongo kadhaa. Wanachama wa makundi haya wanatambuliwa kwa kujichora TATOO karibu mwili mzima! Tattoo kwao ni sehemu ya utambulisho, tattoo yako ndiyo inasema wewe ni mwanachama wa kundi gani la uhalifu!