×

Rais Samia Afunguka Mipango Mikubwa Aliyonayo Tanga ya Viwanda – (Picha+Video)

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwahutubia wananchi wa Mkoa wa Tanga katika muendelezo wa ziara yake ya kikazi mkoani humo tarehe 28 Februari, 2025.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ameeleza matamanio yake kwa mkoa wa Tanga, akisema serikali yake imeanza taratibu za kurejesha Tanga ya viwanda pamoja na kukuza utalii wa fukwe, historia na utamaduni.

Wananchiwakiwa kwenye mkutano wa hadhara wa Rais wa Samia uliofanyika katika uwanja wa Mkwakwani mkoani Tanga.

Wakati akizungumza na wakazi wa Tanga kwenye Uwanja wa Mkwakwani Jijini Tanga Februari 28, 2025, Rais Samia aliyeingia siku yake ya sita ya ziara mkoani humo, amesema ili kufanikisha jambo hilo serikali yake imeendelea kulegeza na kufanya masharti ya uwekezaji kuwa rahisi zaidi kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi ili kuwezesha utanuzi wa viwanda vilivyopo, kukarabati na kujenga viwanda vipya mkoani humo.

Rais Samia akiwasili katika uwanja wa Mkwakwani kwa ajili ya kuwahutubia wananchi mkoani Tanga.

Lengo la kufanya hivyo kulingana na Rais Samia ni kuendelea kukuza fursa za ajira mkoani humo pamoja na kuzalisha ajira mpya kwa vijana, akiwataka wazazi na walezi kuwaepusha vijana na watoto dhidi ya matumizi ya dawa za kulevya kutokana na kuua nguvu kazi ya jamii.

Aidha Rais Samia ameeleza mkakati wake wa kukuza utalii wa fukwe historia na utamaduni mkoani humo kwa kueleza kuwa maumbile ya Tanga, milima, fukwe na utajiri wa kihistoria uliopo mkoani Tanga ni fursa nyingine muhimu kwaajili ya wananchi wa mkoa huo.

Amewahimiza wananchi wa Tanga kuchangamkia fursa hizo zinazoibuliwa mkoani humo, akihimiza pia vijana kujifunza taaluma za uongozaji wa utalii, kufungua kampuni za uwakala wa forodha pamoja na kufungua kampuni za watalii kwenye mkoa huo.