
Rais wa Marekani, Donald Trump, usiku wa kuamkia leo, Machi 5, 2025, alikumbana na upinzani mkali wakati wa hotuba yake kwa Bunge la Marekani.
Hotuba hiyo ilikatizwa mara kwa mara na kelele za kupinga kutoka kwa wabunge wa chama cha Democratic, hali iliyosababisha kutolewa nje kwa Mwakilishi Al Green wa chama hicho.
Katika dakika za mwanzo za hotuba hiyo, wabunge wa upinzani walisikika wakiimba, “USADI! USAID,” na Mwakilishi Al Green (D-Texas) alisimama, akapaza sauti na kutikisa fimbo yake kuelekea kwa Trump huku akisema kwa sauti:
“Huna mamlaka ya kupunguza misaada ya matibabu!”
Kitendo hicho kilimfanya Makamu wa Rais JD Vance kuonekana akimnong’oneza Spika wa Bunge, Mike Johnson, akisema, “Mtoe nje.” Johnson aliingilia kati, akisitisha hotuba ya Trump na kuwataka wabunge kudumisha utulivu.
Spika Johnson aliwakemea wabunge, akiwataka kudumisha nidhamu na kuepuka vurugu ndani ya Bunge.
Baada ya Green kuonekana kupuuza agizo hilo, Johnson alimuagiza Afisa wa Usalama wa Bunge kumtoa nje ya ukumbi, hali iliyosababisha shangwe kubwa kutoka kwa wabunge wa Republican.
Kauli ya Green ilihusiana na pendekezo la Bajeti ya Republican linaloungwa mkono na Trump, ambalo linapendekeza kupunguza mpango wa bima ya afya kwa watu wa kipato cha chini (Medicaid).
Wakati kamera zikiangaza ukumbini, kundi la wabunge wa Democrat kadhaa akiwemo Rashida Tlaib, Maxwell Frost, na Ayanna Pressley walionekana wakiwa wameshika mabango yenye maandishi kama “Uongo,” “Musk anapora,” na “Linda Medicaid.”
Tlaib pia alionekana akiwa ameshikilia ubao mweupe ulioandikwa “Huo ni uongo.”