
Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (BAKWATA) limewatangazia Waislamu na wananchi wote kwa ujumla kuwa Sikukuu ya Eid El-Fitri itakuwa tarehe 31/03/2025 au 01/04/2025 kutegemea mwandamo wa mwezi na kubainisha kuwa Sherehe za Eid El-Fitri kitaifa kwa mwaka huu zitafanyika Mkoa wa Dar es Salaam.
Taarifa ya Machi 22, 2025 iliyotolewa na Katibu mkuu wa BAKWATA, Alhaj Nuhu Jabiri Mruma imeeleza kuwa Swala ya Eid itaswaliwa katika Msikiti wa Mfalme Mohamed VI BAKWATA Makao Makuu Kinondoni kuanzia saa 1.30 asubuhi na kufuatiwa na Baraza la Eid litakalofanyika katika Ukumbi wa Mwalimu Nyerere kuanzia saa 09.00 mchana Inshallah.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa Mgeni Rasmi katika Baraza la Eid atakuwa Mheshimiwa Dk. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania huku Waislamu wote wakiombwa kuhudhuria kwenye Ukumbi kwa wingi na kwa wakati.
“Kwa niaba ya Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania Mh. Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania Dr. Sheikh Abubakar Zubeir bin Ally Mbwana anawatakia Swaumu njema katika kumi la mwisho la mwezi Mtukufu wa Ramadhani na maandalizi mema ya Sikukuu ya Eid el-fitri”——imesema taarifa hiyo