×

Rais Mstaafu Kikwete Awasilisha Ujumbe Maalum Wa Rais Samia Kwa Rais Wa Gambia

Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete (kulia) akisalimiana na Adama Barrow, Rais wa Jamhuri ya Gambia. 

RAIS Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete, Machi 26, 2025 amewasilisha Ujumbe Maalum kutoka kwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa Adama Barrow, Rais wa Jamhuri ya Gambia. Mazungumzo kati ya viongozi hao yamefanyika Ikulu ya Gambia, jijini Banjul.

Akiwasilisha ujumbe huo, Kikwete ameelezea uhusiano mzuri wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Gambia, na dhamira ya Rais Samia ya kuimarisha zaidi ushirikiano huo kwa manufaa ya wananchi wa pande zote mbili.

Kwa upande wake, Rais Barrow amepongeza uongozi thabiti wa Rais Samia, si tu ndani ya Tanzania bali pia katika Bara la Afrika kwa ujumla. Ameeleza furaha yake kwa kumkaribisha Rais Mstaafu wa Tanzania katika Ikulu ya Gambia na kusisitiza kuwa Tanzania ni mfano bora wa uongozi wenye utulivu na demokrasia imara barani Afrika.

Aidha, Rais Barrow amepongeza utamaduni wa kisiasa wa Tanzania, ambapo viongozi wakuu hukabidhiana madaraka kwa amani na utulivu, akieleza kuwa ujio wa Rais Mstaafu Kikwete kama Mjumbe Maalum wa Rais Samia ni ishara ya ukomavu wa siasa na utawala bora nchini Tanzania.

Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete akiongea jambo.