
Serikali kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo imetangaza rasmi kufungwa kwa muda wa Uwanja wa Benjamin Mkapa ili kupisha marekebisho katika eneo la kuchezea (pitch) ambalo limeharibika vibaya kutokana na mvua kubwa zilizonyesha hivi karibuni.
Katika taarifa iliyotolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, imeelezwa kuwa mvua hizo zilizoambatana na mechi ya Robo Fainali ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika kati ya Simba SC na Al Masry ya Misri zimesababisha athari kubwa katika uwanja huo.
Wizara imesema timu ya wataalamu itaingia mara moja kufanya tathmini ya kina kuhusu kiwango cha uharibifu na muda ambao marekebisho yatakamilika kabla ya kutangaza tarehe rasmi ya kufunguliwa tena kwa uwanja huo.
Aidha, timu zote zilizopanga kutumia uwanja wa Benjamin Mkapa kwa mechi za kitaifa na kimataifa zimetakiwa kutafuta viwanja mbadala kwa muda, huku serikali ikisisitiza kuwa marekebisho yatafanyika kwa haraka ili kurejesha hali ya kawaida.
Wizara imetoa pole kwa usumbufu utakaojitokeza kwa wadau wa michezo na wananchi kwa ujumla kutokana na hatua hiyo ya dharura, ikiahidi kushughulikia changamoto hiyo kwa haraka.
