×

Simba Watua Morocco Kibabe kwa Ajili ya Mchezo wa Fainali

Kikosi cha Simba chawasili salama nchini Morocco kwa ajili ya mchezo wa mkondo wa kwanza wa fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika (CAFCC) dhidi ya RS Berkane. Timu hiyo iliwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mohammed V, jijini Casablanca, baada ya safari ya saa kadhaa iliyochukua takriban masaa tisa kutoka Dar es Salaam.

Safari hiyo ilianza rasmi saa 3:00 usiku wa Jumanne ambapo wachezaji, benchi la ufundi na viongozi wa Simba waliondoka nchini Tanzania wakiwa na ari na morali ya hali ya juu kuelekea katika mchezo huo muhimu.

Mchezo huo wa kwanza wa fainali unatarajiwa kuchezwa Mei 17, 2025, kuanzia saa 4:00 usiku kwa saa za Afrika Mashariki, kwenye Uwanja wa Berkane, Morocco. Huu utakuwa ni mtihani mkubwa kwa Simba SC, ambao wanaendelea kujivunia rekodi nzuri katika mashindano haya msimu huu.

Kocha mkuu wa Simba, Robert Oliveira, ameweka wazi kuwa kikosi chake kiko tayari kwa mapambano na ana matumaini makubwa ya kupata matokeo chanya ugenini kabla ya mchezo wa marudiano utakaochezwa Dar es Salaam.

Mashabiki wa Simba SC wamekuwa na hamasa kubwa, wakiamini kuwa kikosi chao kina uwezo wa kufanya vizuri na kuweka hai matumaini ya kutwaa taji hilo la kihistoria. Huku wenyeji RS Berkane nao wakijiandaa kwa mapambano makali nyumbani kwao.

Macho na masikio ya mashabiki wa soka barani Afrika yatakuwa yameelekezwa Morocco katika mchezo huo wa kusisimua ambao utatoa mwelekeo wa nani atakayetwaa ubingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu.