
Mwanamuziki maarufu na mfanyabiashara Sean “Diddy” Combs, mwenye umri wa miaka 55, ambaye anakabiliwa na mashtaka mazito mahakamani ya unyanyasaji wa kingono, ulaghai, usafirishaji wa watu kwa ajili ya ukahaba, na kuendesha mtandao wa uhalifu wa kijinsia, kulingana na taarifa zilizotolewa katika mahakama ya Marekani imeanza kuunguruma jana na leo inaendelea kusikilizwa.
Katika ufunguzi wa kesi hiyo jana , waendesha mashtaka walidai mahakamani hapo kuwa Diddy alitumia umaarufu wake, kuwadhibiti wanawake – hususan wapenzi wake wa zamani, akiwalazimisha kushiriki vitendo vya ngono visivyo kwa ridhaa, ambavyo alivirekodi na kuvihifadhi.
Ushahidi wa video uliotolewa jana unaomuonesha Diddy akimpiga na kumburuza mpenzi wake wa zamani, Cassandra Ventura, katika hoteli moja jijini Los Angeles mnamo mwaka 2016, umekuwa kitovu cha kesi hii.
Mlinzi wa hoteli hiyo alithibitisha kuwa video hiyo ni ya kweli, na tayari imesambaa mitandaoni.
Mwendesha mashtaka Emily Johnson alisema kuwa Diddy alikuwa akiwadhibiti wanawake kupitia hofu na ushawishi wa kimuziki, na aliendesha kile alichokiita “freak-offs” — tafrija za ngono ambazo zilitumika kama njia ya unyanyasaji na udhibiti wa kisaikolojia.

Shahidi mwingine, Daniel Phillip, meneja wa zamani wa watumbuizaji, alisimulia kuwa alishinikizwa kushiriki ngono na Bi Ventura kwa zaidi ya saa 10, huku Diddy akitazama na kurekodi.
Phillip alisema aliogopa kutoa taarifa polisi kutokana na hofu ya kuuawa au kutekwa, akieleza kuwa Diddy ni mtu mwenye “nguvu kubwa na ushawishi usio wa kawaida.”
Alieleza pia kuwa alishuhudia Diddy akimshambulia Bi Ventura zaidi ya mara moja, na mara moja alimvuta nywele kwa nguvu huku akilia kwa sauti.
Kwa upande wao, mawakili wa Diddy wamesema kuwa video hiyo inathibitisha kuwa mshtakiwa ana “tabia yenye kasoro,” lakini siyo uhalifu wa kuendesha biashara ya ngono. Wakili Teny Geragos alisema, “Unyanyasaji wa majumbani sio biashara ya ngono.”
Kesi hii imevuta hisia za watu duniani kote na imeendelea leo Jumanne, ambapo Ventura mwenyewe ametoa ushahidi wake.