
Kila mwaka ifikapo tarehe 26 ya mwezi Aprili, dunia huadhimisha siku ya miliki ubunifu. Siku hii ilianza kuadhimishwa rasmi mwaka 2000 na Shirika la Miliki Ubunifu Duniani (WIPO), ili kuenzi na kuthamini mchango wa miliki bunifu katika maendeleo na kutatua changamoto zinazoikabili jamii.
Vilevile, kukuza uelewa kuhusu usajili, ulinzi, haki za miliki ubunifu na kukuza ubunifu na uvumbuzi katika nyanja mbalimbali.
Tarehe 26 Aprili kwa Tanzania ni sikukuu ya maadhimisho ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, hivyo maadhimisho ya siku ya miliki ubunifu hufanyika kwa tarehe nyingine lakini lengo likiwa ni lile lile bila kuathiri dhima au ujumbe uliokusudiwa na WIPO kwa mwaka husika.

Muziki ni lugha inayoweza kuzungumzwa na yeyote kupitia mdundo na mahadhi ya muziki unaotumbuiza. Hii inaweza kuwa ni kupitia muziki wa jadi mpaka muziki wa kisasa au muziki mambo leo. Ala za muziki peke yake zinaweza kuburudisha na zikabeba ujumbe.
Kadhalika, wimbo unaweza kuimbwa kwa lugha ya kigeni ambayo mtu haifahamu, bado anaweza kuburudika na kuufurahia muziki. Mojawapo ya nadharia za muziki ni kuwa, muziki ni lugha inayoeleweka na binadamu wote.
Uvumbuzi na ubunifu wa binadamu ndiyo vitu vinavyoiendesha dunia. Ndiyo vitu vinavyoshamirisha katika kuiboresha dunia.
Uvumbuzi na ubunifu hujumuisha masuala ya sayansi na teknolojia, usanifu wa majengo na maumbo mbalimbali ambayo hutumika katika mazingira yanayomzunguka binadamu. Sanaa ni sehemu ya ubunifu ambao binadamu hutumia katika kufunza, kuadilisha, kuhaulisha maadili ya jamii kutoka kizazi kimoja kwenda kingine.
Pamoja na hayo, sanaa hutumika kuburudisha, kufariji na kuliwaza lakini pia kutunza kumbukumbu za jamii. Sanaa pia hutumika kama utambulisho wa jamii na utambulisho wa taifa kwa ujumla. Zaidi, sanaa hutumika kama njia ya kumuongeza mbunifu kipato hivyo kuongeza pato la Taifa.
Shirika la Miliki Ubunifu Duniani kwa kutambua umuhimu wa sanaa kama moja wapo ya bunifu nyingi zilizopo katika jamii, likaona ni vema kwa mwaka huu 2025 kutambua umuhimu wa sanaa ya muziki katika kulinda na kukuza ubunifu duniani.
Lengo la kuanzishwa kwa siku hii ni kuenzi na kutambua mchango wa wabunifu na wavumbuzi katika kuchangia maendeleo kijamii na kiuchumi. Kauli mbiu ya siku ya miliki ubunifu duniani mwaka huu ni “Miliki Ubunifu na Muziki: Sikilizia Mdundo wa Ubunifu”, (IP and Music: Feel the Beat of IP).
Muziki ni kazi ya sanaa yenye upekee katika jamii ya binadamu. Muziki hutumika kuhamasisha, kuadilisha, kutambulisha jamii kupitia midundo na mahadhi yake ambapo mahadhi ya muziki wa jamii moja hutofautiana na ya jamii nyingine, hivyo kuzitofautisha jamii hizo.
Kubwa na la muhimu zaidi, mahadhi na midundo ya muziki kutoka kizazi kimoja na kwenda kizazi kingine hubadilika. Hivyo muziki hutofautisha kizazi kimoja na kingine. Naam, huu ndiyo upekee wa muziki.
Pamoja na hayo yote, muziki ulianza kama burudani tu ambayo ilitumika kumliwaza binadamu wakati wa huzuni, pia ulitumika kumburudisha binadamu pindi anapokuwa amechoka vile vile ulitumika kuleta kumbukumbu ya nyakati ambazo binadamu amezipitia katika maisha yake.
Kwa mantiki hiyo, muziki umekuwa ni kiunganishi cha nyakati mbalimbali ambazo binadamu amezipitia katika kukabiliana na mazingira yake.
Kutokana na mabadiliko ya nyakati kiteknolojia na kiuchumi muziki umehama kutoka kuwa sehemu tu ya burudani inayopatikana bure na kuwa bidhaa inayoweza kumuingizia binadamu kipato na kubadilisha maisha ya mtu mmoja mmoja na kuchangia pato la jamii au taifa kwa ujumla wake.
Kama nilivyodokeza hapo juu kuhusu siku ya miliki ubunifu duniani mwaka 2025 na kauli mbiu yake, WIPO inatambua kwamba muziki ni sehemu muhimu sana katika maendeleo ya miliki ubunifu.
Muziki upo karibu katika kila uwanda wa maisha ya binadamu na unachangia ukuaji na uzalishaji wa aina nyingine za bunifu na vumbuzi. Licha ya kwamba muziki hulindwa kwa utaratibu wa sheria za Hakimiliki na Hakishiriki, lakini haipingiki kwamba, muziki umechangia sana kukuza uvumbuzi wa kiteknolojia katika maeneo mbalimbali.
Kazi za sanaa ikiwemo muziki zina stahili kulindwa kwa mujibu wa sheria ili ziweze kuleta tija ya kiuchumi katika jamii. Muziki ni kazi ya ubunifu ambayo ni rahisi sana kuhujumiwa au kuibiwa ukilinganisha na aina nyinginezo za miliki ubunifu.
Ni ukweli usiopingika kwamba, muziki hauhitaji teknolojia kubwa kama aina nyingine za miliki bunifu ambazo zinahitaji rasilimali kubwa ili kuweza kuzalisha. Hivyo, wahalifu wanaofanya uharamia wa miliki bunifu za aina nyingine hulazimika kutumia rasilimali nyingi ambazo pia ni gharama kuweza kufanikisha uharamia huo.
Hii ni tofauti na kazi za muziki ambazo uharamia wake ni kazi rahisi ambapo wanaofanya uharamia huo hupata faida kubwa bila kutoa jasho kama ambavyo mtunzi wa muziki anavyotoa jasho kuandaa kazi yake.
Maendeleo ya sayansi na teknolojia yamerahisisha uharamia wa kazi za muziki ambapo wahalifu hutumia teknolojia hasa TEHAMA kujinufaisha na jasho la wanamuziki kwa kuuza au kurudufu kazi za muziki bila ridhaa ya wasanii au wamiliki wa kazi za muziki hizo.
Utatuzi wa changamoto hii hautegemei sana uwepo wa sheria pekee katika kutatua changamoto hiyo, bali unategemea zaidi uelewa na utayari wa jamii nzima kulinda na kuheshimu kazi za muziki na kuzipa thamani inayotakiwa ili kuwanufaisha wanamuziki na pia jamii nzima na taifa kwa ujumla kunufaika.
Tofauti na miaka ya zamani ambapo usambazaji wa kazi za muziki ulitegemea sana uuzwaji wa santuri, kanda za muziki na baadaye kuwepo kwa vibebeo kama diski gandamize/ diski songamano (CD), diski mweko (flash disk) na hata simu janja (Smart phone) kwa sasa.
Mabadiliko ya teknolojia yamepelekea usambazaji wa kazi za muziki kuhama kwa urahisi kutoka katika vifaa ambavyo ni vya kubeba na kwenda kwenye majukwaa ya kidijiti ambayo wamiliki wake hawakutani uso kwa uso na wamiliki wa muziki kwa ajili ya kufanya makubaliano ya kuuziana na kupeana mikataba ya kusambaza kazi hizo za muziki.
Wakati mabadiliko hayo yakitokea, sheria zinazolinda maslahi na haki za wabunifu wa kazi za muziki zinakuwa bado hazijabadilika ili kwenda sambamba na mabadiliko ya teknolojia.
Pia, kwa namna nyingine hata wabunifu wa kazi za muziki wanakuwa ama wao wenyewe hawapati fursa ya kutosha kujifunza athari, au manufaa ya kutumia majukwaa hayo kusambaza kazi zao. Matokeo yake wabunifu wa kazi za muziki hawanufaiki ipasavyo na uwekezaji wao wanaoufanya katika kuzalisha na kutengeneza muziki wao ukilinganisha na wamiliki wa majukwaa ya uzalishaji wa muziki huo. Kadhalika, majukwaa hayo yamerahisisha zaidi uhalifu na uvunjifu wa hakimiliki na hakishiriki za wabunifu wa sanaa za muziki.
Kwa kuhitimisha, mada ya “Miliki Ubunifu na Muziki: Sikiliza Mdundo wa Miliki Ubunifu” inatualika kusherehekea muziki kama nguvu inayoziunganisha jamii lakini pia tuzilinde haki za miliki bunifu zinazoambatana na muziki.
Wakati teknolojia na tamaduni zikiendelea kubadilika, hakimiliki na hakishiriki za wabunifu wa muziki zitaendelea kubaki na zinapaswa kuheshimiwa na kila mmoja wetu. Tuungane na ulimwengu mzima kuthamini wabunifu wa muziki na kukuza mazingira yanahohimiza ubunifu wa muziki na teknolojia katika muziki. MAKALA HII IMELETWA NA NEEMA ADRIAN