
Dar es Salaam 4 Julai 2025: Katika Maendeleo ya Sayansi na Teknolojia, Wasomi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) mwaka huu kwenye Maonesho ya Kibiashara ya Kimataifa ya 49 ya Sabasaba yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar, wamekuja na mtambo wa kisasa wa kuchejua madini.
Akizungumza na Global Tv Mwanafunzi wa UDSM, Shule Kuu ya Madini, Malemi Joseph amesema mtambo huo mpya walioubuni, umekuja kuwa mkombozi kwa kuwarahisishia kazi wachimbaji wadogo wa dhahabu.

“Mtambo huu umekuja kwa ajili ya kuondoa changamoto walizokuwa wakikumbana nazo wachimbaji wadogo katika shughuli zao za kila siku katika uchimbaji.
“Miongoni mwa changamoto zilizotatuliwa na mtambo huu kwanza kabisa umekuja kupunguza gharama za uendeshaji kwa maana ya kuondoa gharama za kutumia dawa kwa ajili za kuchenjulia dhahabu.
Mtambo huu pia una kasi kubwa ya kuchuja na kuchenjua dhahabu hivyo kuokoa muda na kufanya kiasi cha dhahabu kupatikana kwa wingi kuliko awali”. Alimaliza kusema mwanafunzi huyo.
HABARI/PICHA: RICHARD BUKOS NA NEEMA ADRIAN /GPL