
TBA Yaelezea Miradi inayoitekeleza kama Wakala wa Majengo hapa nchini na kuwashauri wananchi kuwatumia wataalamu bora kutoka TBA kwa ujenzi bora na uhakika na kuachana na ujenzi wa kienyeji uliopitwa na wakati pamoja na kwenda kuwekeza kwenye majengo yao.

Akizungumza na Global Tv kwenye Maonesho ya 49 ya Kibiashara ya Kimataifa maarufu Sabasaba ambayo yanafanyika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar, Mtumishi wa Wakala wa Majengo Tanzania, John Mboya amewashauri wananchi kuwatumia TBA kwa ujenzi bora na wa uhakika.
Mboya alianza na kuwaelezea wananchi waliofika kwenye banda lao lililopo kwenye viwanja hivyo miradi mbalimbali wanayoendelea kushughulika nayo kwa hapa jijini kuwa ni pamoja na mradi wa Canadian ambao kwasasa una majengo matatu ambayo yameshajengwa ambapo jengo moja tayari limeshakamilika na mengine yapo kwenye hatua za mwishoni.

Mboya aliulezea mradi mwingine ulipo Magomeni Kota katika Halmashauri ya Wilaya ya Kinondoni Dar, na kusema mradi huo una majengo manne yenye floor nane kila moja ambapo mawili tayari yameshakamilikia na watu wanaishi na hayo mawili mengine yapo hatua za mwishoni.
Mboya alisema wanawakaribisha wadau kufika kwenye miradi kwa ajili ya kujifunza ili kujionea miradi yao inavyotekelezwa.
Baada ya miradi hiyo Mboya alimalizia kuulezea na mradi wao wa Temeke ambao unaitwa Temeke Kota na kuendelea kusema;
“Huu mradi wa Temeke Kota ni moja kati ya miradi yetu mikubwa sana tunayoitekeleza ambao unatarajiwa kuchukua familia zaidi ya 120, na mpaka sasa tumefikia floor ya nne na bado tunaendelea maana linatarajiwa kuwa na floor tisa.
“Hivyo tunategemea kulikamilisha kwa wakati ili kuwahudumia wananchi ikiwemo watumishi wa umma na watu binafsi.” Alimaliza kusema Mboya.

Kwa upande wake Mkadiliaji Majengo wa TBA, Paulina Ngalai amesema wanawakaribisha sana wananchi kwenye banda lao lililopo kwenye maonesho hayo na kueleza kuwa kazi yao kubwa ni kuzingatia ubora wa majengo, kufanya usanifu, ubunifu na ukadiriaji.
“Mwananchi ukishaingia kwenye banda letu utakutana na wataalamu mbalimbali na kujifunza mambo mbalimbali yanayohusu masuala ya ujenzi.
Mkadiriaji huyo majengo alisema wananchi wengi wamekuwa na mazoea ya kuanza ujenzi kwa kuwahusisha watu mbalimbali na kumsahau mkadiriaji majengo ambaye ataweza kukupa thamani ya nyumba unayotarajia kuijenga kukufanya ujiandae na si kujijengea tu kienyeji”. Alimaliza kusema.

Naye Afisa Miliki wa TBA, Kelvin Rugazia amesema katika idara ya milki TBA wanazo fursa nyingi na nzuri kwa ajili ya wananchi na wana ofisi sehemu mbalimbali hapa nchini ambapo katika ofisi hizo mwanachi yeyote anaweza kufika na kupata fursa zilizopo haswa katika sehemu ya milki.

“Tunajenga nyumba kwa ajili ya wapangaji na kwa watumishi wa umma na pia tuna nyuma maeneo ya mjini kwa ajili ya upangishaji kwa ajili ya wafanyabiashara.
“TBA pia tumeweza kuainisha katika kipindi hiki maeneo ambayo yapo tayari kwa ajili ya uwekezaji katika mikoa ya Dar es Salaam, Arusha, Dodoma na Mwanza tuna maeneo mazuri kwa ajili ya uwekezaji ambayo tunaweza kuingia ubia na yeyote yule aliyetayari kwa ajili ya kuwekeza.
“Hivyo basi nawakaribisha wananchi kwenye banda letu la maonesho kwa ajili uwekezaji na mambo mengineyo”. Alimaliza kusema Afisa Milki Rugazia. HABARI/PICHA: NEEMA ADRIAN NA RICHARD BUKOS /GPL