×

Kamishna wa Bima Awakaribisha Wadau Kijiji cha Bima Kwenye Maonesho ya Sabasaba

Kamishna wa Bima nchini, Dkt. Baghayo Saqware amewakaribisha wananchi kufika Kijiji cha Bima kilichopo kwenye Maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya 49 yanayoendelea katika Viwanja vya Julius Nyerere maarufu Sabasaba jijini Dar, kujipatia huduma mbalimbali kwenye kijiji cha bima kilichowakusanya mawakala mbalimbali wa huduma za bima.

Akizungumza na wanahabari Kamishna Saqware alisema mwaka huu wameamua kuja na mpango Kijiji cha Bima ili kutoa huduma za bima kwa wananchi kwa pamoja.

Kamishna huyo aliendelea kusema;

“Nimefurahi kufika hapa katika kijiji cha bima ambapo kuna wadau wa kutoa huduma za bima zaidi ya 30 wamekusanyika hapa kwa lengo la kutoa huduma na elimu ya bima.

“Kamishna huyo amesema sambamba na watoa huduma hao pia kwenye banda la kijiji cha bima wapo na Mamlaka ya Usimamizi wa Bima hapa nchini (TIRA) ambayo inajukumu la kusikiliza malalamiko na changamoto zingine mbalimbali zinazohusu bima na kutoa elimu ya bima.

“Kamishna Saqware amesema kwenye kijiji hicho zinatolewa huduma za aina zote kama bima ya maisha, bima ya mitambo, uwekezaji, majengo, fedha, biashara na nyinginezo.

“Kupitia msimamizi wa bima yaani TIRA ambaye ndiye msajili wa wakala wa bima wananchi wataweza kupata huduma mbalimbali za kibima ikiwemo kupata huduma za bima, elimu ya bima pia kupokea malalamiko mbalimbali ya bima”. Alimaliza kusema Kamishna Saqware na kuendelea kukagua mabanda ya mawakala wa bima kwenye kijiji hicho.