
Kocha wa zamani wa Real Madrid, Carlo Ancelotti, amehukumiwa kifungo cha mwaka mmoja gerezani na kutozwa faini ya €386,000 (zaidi ya TSh 1.1 bilioni) na Mahakama ya Mkoa wa Madrid kwa kosa la kukwepa kodi mwaka 2014 alipokuwa katika kipindi chake cha kwanza kuifundisha Real Madrid (2013–2015).
Ancelotti (65), ambaye sasa ni kocha wa timu ya taifa ya Brazil, alidai kuwa hakuwa na nia ya kudanganya mamlaka za kodi za Uhispania na kwamba Real Madrid walipaswa kushughulikia makato ya kodi za mapato hayo.
Awali, waendesha mashtaka walipendekeza ahukumiwe kifungo cha miaka 4 na miezi 9 pamoja na faini ya €3.2 milioni (zaidi ya TSh 9.3 bilioni), lakini mahakama ilitoa uamuzi tofauti baada ya kusikiliza ushahidi mwezi Aprili 2025.
Hata hivyo, Ancelotti hatarajiwi kutumikia kifungo hicho, kwani chini ya sheria za Uhispania, hukumu ya chini ya miaka miwili kwa makosa yasiyo ya vurugu kwa mara ya kwanza huwa inasamehewa kwa masharti.