
Klabu ya Simba SC ipo kwenye nafasi nzuri ya kukamilisha usajili wa kiungo chipukizi wa CS Sfaxien ya Tunisia, Balla Moussa Conté mwenye umri wa miaka 21, huku wakiwazidi kete watani wao wa jadi, Yanga SC.
Jana mchana, kulikuwepo na makubaliano ya awali kati ya CS Sfaxien na Yanga, yaliyowapa Yanga ruhusa ya kuzungumza na mchezaji huyo kabla ya makubaliano ya kibinafsi kufikiwa. Hata hivyo, usiku wa jana mambo yalibadilika ghafla baada ya Simba kuwasilisha ofa kubwa zaidi kwa klabu ya Tunisia na kuingia moja kwa moja kwenye mazungumzo na mawakala wa mchezaji kupitia kocha wao, Fadlu Davids.
Inaelezwa kuwa kocha Fadlu amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha Simba inamnasa kiungo huyo, akimtaja kuwa ndio chaguo lake la kwanza katika dirisha hili la usajili. Mazungumzo ya moja kwa moja baina ya Fadlu na mawakala wa Conté yameleta mabadiliko makubwa kwenye mwelekeo wa uamuzi wa mchezaji huyo.
Ingawa Yanga SC bado wanaendelea ku-push kukamilisha makubaliano na mchezaji, kwa sasa Conté anaelezwa kuwa amelalia upande wa Simba SC, kufuatia mazungumzo ya moja kwa moja aliyofanya na kocha Fadlu.
Balla Moussa Conté, ambaye amekuwa na msimu mzuri akiwa na CS Sfaxien, anatajwa kuwa na uwezo mkubwa wa kucheza kama kiungo mshambuliaji au mchezeshaji wa kati — nafasi ambazo timu zote mbili za Tanzania zinahitaji kuziboresha kuelekea msimu wa 2025/2026.