
Rais wa Klabu ya Simba SC, Mohammed Dewji, ameuvunja ukimya na kuwahakikishia mashabiki wa klabu hiyo kuwa timu yao ipo kwenye mwelekeo sahihi, licha ya changamoto zilizowakumba msimu uliopita.
Kupitia ujumbe wake rasmi kwa wapenzi wa Simba, Dewji amesema anafahamu kuwa mashabiki wamebeba maswali mengi mioyoni mwao, lakini amesisitiza kuwa huu si wakati wa lawama, bali ni kipindi cha umakini, mshikamano, na kuchukua hatua za kweli.
“Kupambania Simba ni wajibu wangu. Huu siyo wakati wa lawama, ni wakati wa kusimama imara, kuwa kitu kimoja na kuchukua hatua sahihi za kuleta mabadiliko chanya,” amesema Dewji katika taarifa yake ya Oktoba 6, 2024.

Rais huyo ameeleza kuwa Simba ipo katika kipindi cha mpito, na tayari hatua muhimu zimechukuliwa — ikiwemo kujenga kikosi kipya, kuimarisha benchi la ufundi, na kuweka msingi wa mwelekeo mpya kwa ajili ya mafanikio ya baadaye.
“Msimu huu tumefika mbali zaidi ya matarajio, na msimu ujao tunarudi kwa nguvu mpya,” aliongeza.
Aidha, Dewji ameahidi kuwa siku chache zijazo atazungumza moja kwa moja na mashabiki, akifichua kuwa kuna kazi kubwa inaendelea nyuma ya pazia na kwamba matumaini ya kweli yapo.
Akamaliza kwa wito wa mshikamano:
“Naomba tuendelee kuwa wavumilivu. Tunahitaji kufanya marekebisho makubwa. Tuendelee kusimama pamoja kama familia moja. Mbele yetu kuna mwanga.”