
Dar es Salaam, 21 Agosti 2025: Kampuni ya ORYX Energies Tanzania kwa kushirikiana na Serikali na wadau wa soko, imetangaza rasmi uzinduzi wa mfumo wa kwanza wa usambazaji wa gesi ya LPG kwa wingi katika Soko la Samaki la Kimataifa Ferry jijini Dar es Salaam.
Mradi huo wa kihistoria ni hatua kubwa katika kuimarisha upatikanaji wa nishati safi kwa wauzaji wa samaki na wajasiriamali wadogo katika soko hilo ambapo sasa mfumo huo unaweza kulipia kadri ya matumizi (PAYG), unaowawezesha wauzaji kulipia gesi wanayotumia tu na hivyo kuondoa gharama kubwa za kujaza mitungi na kupunguza matumizi ya kila siku hadi Sh.45,000.

Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa mfumo huo ambapo limejengwa tanki kubwa ambalo linatumika kusambaza gesi katika majiko ya wafanyabiashara hao, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila amesema mfumo huo sasa utawezesha kulipa kulingana na matumizi yako.
Amesema ajenda ya kuwa na matumizi ya nishati safi ya kupikia ilikuwepo tangu zamanı lakini mkazo wake ulikuwa mdogo lakini Rais Dk.Samia Suluhu Hassan ameibeba ajenda hiyo na Oryx Energies wameonesha kwa vitendo kuunga mkono jitihada hizo kwa kuendelea kuhamasisha matumizi ya nishati hiyo.

“Wenzetu Oryx Energies kwa kuendelea kujitoa kwao katika eneo hili la nishati safi ya kupikia kwa kuja na Mfumo huu ambao sasa unakwenda kurahisisha upatikanaji gesi katika soko hili la samaki feri.
“Hapa katika Soko la samaki feri kuna majiko ya wakaanga samaki 48 na sasa wote wameunganishwa katika mfumo huo wa gesi na tunaamini matumizi ya nishati safi ya kupikia yanakwenda kuokoa hata changamoto za kiafya za watumiaji wakiwemo wanawake ambao wanafanya shughuli zao katika soko la samaki feri .

Amefafanua matumizi ya nishati safi ya kupikia hayaokoi tu afya za watumiaji bali hata gharama za uendeshaji zinapungua kwa asiliamia kubwa na kuongeza mradi huo umegharimu zaidi ya Sh.milioni 250 na matamanio yake ni kuona masoko yote yalipo katika Jiji la Dar es salaam yanakuwa na mfumo huo.
Akieleza zaidi amesema hawazindui tu miundombinu bali wamezindua mabadiliko ya kweli katika usalama, ufanisi, na ustawi wa kila mfanyabiashara anayefanya kazi hapa sokoni. Kupitia mradi huo Oryx wameweka matanki ya gesi chini ya ardhi, vaporizers, na mtandao wa mabomba unaohudumia majiko yote 48

Amesema kila mfanyabiashara sasa ana mita yake inayosoma matumizi yake ya kila siku, kabla na baada ya matumizi. Hakuna tena kubahatisha, hakuna tena kulazimika kununua mitungi midogo kwa gharama kubwa.
Pia amesema Oryx wamezingatia usalama,kwa kufunga valve ambazo itatumika kufunga gesi endapo itatokea dharulakwa kila jiko. Tunafahamu matumizi makubwa hivi ya gesi yanahitaji usalama wa hali ya juu.
“Nafahamu kwamba Oryx mtaendelea kutoa elimu ya matumizi sahihi ya huu mfumo ilikuepusha ajali yoyote inayoweza kutokea kwa kutokujua aukupuuzia kanuni sahihi za usalama. Nimeambiwa pia kuwa mradi huu ni ufadhiri wa asilimia 100 toka kwenu Oryx energies na mmetumia zaidi ya Sh.milioni 250.
Akifafanua zaidi amesema kuwa faida za matanki ya gesi yaliyofungwa yanaondoa usumbufu wakubadilisha kubadilisha ile mitungi midogo midogo mara kwa mara, gesi pia itapatikana inapatikana bila usumbufu.
Pia amesema viwango vya matumizi gesi vitafuatiliwa kwa urahisi ili kuhakikisha gesi inaletwa kujaza kwenye hili tanki kubwakwa wakati huku akieleza gharama imepungua na wafanyabiashara waliokuwa wakitumia hadi Sh.180,000 kujaza gesi kwa siku sasa wanaweza kuokoa hadi Sh.45,000 kila siku.
“Kupitia mfumo wa Lipa Kadri Unavyotumia,hili ni suala la kupongezwa sana. Hakuna upotevu, hakuna gesi isiyotumika tofauti na zamani ambapo mtungi mdogo mliotumia wakati fulani gesi inabaki kidogo. Kuhusu usalama, hili sina shaka na utalamu wenu Oryx kwenye suala zima la usalama.”
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Oryx Gas, Benoit Araman amesema lengo la kuwa na tanki la gesi katika soko hilo unalenga kupunguza gharama za kujaza, kupunguza upotevu, na kuongeza ufanisi
Usalama Mfumo usiovuja
Amesema ni mfumo wa kisasa uliofanywa na team ya ufundi ya Oryx gas kwa kuzingatia kanuni za kitaifa na kimataifa.Pia urahisishaji wa Uendeshaji Ugavi endelevu pamoja na ufuatiliaji wa kisasa, na matengenezo madogo.
Kuhusu Dira ya Taifa Kupanua matumizi ya nishati safi Benoit amesema ORYX Energies imejipanga kuunga mkono Mkakati wa Taifa wa Kupikia kwa Usafi 2024–2034, kwa kusambaza mfumo huu katika masoko ya samaki ya Zanzibar, Mwanza, na mikoa mingine.
“Kampuni pia inaendelea kuunganisha hii mifumo ya LPG kwa wingi pia mashuleni, taasisi, majengo ya biashara, naviwanda kote nchini.Mradi huu si miundombinu tu ni ahadi ya kuinua jamii, kulinda mazingira, na kuchochea ukuaji wa uchumi,” alisema.
Awali Kamishina wa Nishati Mhandisi Innocent Luoga kutoka Wizara ya Nishati ameeleza hatua
ambazo zinaendelea kuchukuliwa na Serikali katika kufanikisha mpango wa nishati safi huku akiipongeza Oryx kwa hatua inazoendelea kuchukua katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.