ILIPOISHIA
Mzee Hassani hakutaka kuzungumza tena, naye alikuwa kimya, macho yake yalikuwa mbele, hakuonekana kuwa na hofu hata kidogo, ila kwangu, nilitamani nirudi. Eti huko ndipo kulipokuwa na utajiri! Nikasubiri nione nini kingetokea.
SONGA NAYO…
Tuliendelea na safari mpaka tulipofika sehemu fulani ambayo ilikuwa na miti mingi na kwa mbali kulikuwa na nyumba ndogo ya udongo. Nilibaki na mshangao, sikuamini sehemu kama hiyo kungekuwa na mtu anaishi, niliogopa, wakati mwingine nilihisi kama nilikuwa kwenye sehemu mbaya, yenye kutisha ambayo ingenifanya nitekwe na watu wenye roho mbaya.
“Ila si natafuta utajiri, haina jinsi…” nilijisemea.
Mzee Mudi akaniambia niteremke na tuanze kwenda kule kwenye kile kijumba, wakati natembea, mwili wangu ulikuwa unatetemeka mno na wakati mwingine nilihisi ningeweza hata kuanguka.
“Mbona unatetemeka?” aliniuliza.
“Hakuna kitu.”
“Kweli?”
“Ndiyo!”
Japokuwa nilimficha lakini nilikuwa na uhakika kwamba alinigundua. Tuliendelea kusogea mbele mpaka tulipokifikia kijumba kile ambapo aliniambia kwamba hatukutakiwa kuingia moja kwa moja bali tulitakiwa kusubiri nje, tukafanya hivyo.
Baada ya dakika kama mbili, tukasikia sauti ndani ikitukaribisha, tukasimama na kuanza kuingia. Huko, tulimkuta mzee mmoja, kwa kumwangalia haraka, alikuwa na miaka kama sabini ila alikuwa amechoka sana kimaisha.
Kichwa changu kikaanza kujiuliza, je, mzee yule angeweza kunifanya niwe tajiri kama nilivyotaka? Wakati najiuliza hayo, nikashangaa mzee yule akisimama na kunishika kichwa changu.
“Usijiulize swali hilo, nitakufanya kuwa tajiri mkubwa sana,” aliniambia huku akiwa amenikazia macho.
Kwanza nikashtuka, ilikuwaje ajue kile nilichokuwa nikijiuliza, mpaka hapo, nikajua kwamba huyo mzee alikuwa na nguvu za ziada. Nikatulia na kumwangalia usoni. Kwa jinsi chumba kile kilivyokuwa, kiliniogopesha mno, kulikuwa na tunguri kila kona, harufu mbaya ambayo ilinifanya kutamani kuziba pua zangu.
“Unataka kuwa tajiri?” aliniuliza mzee huyo.
“Ndiyo!”
“Una uhakika?” aliniuliza.
“Ndiyo mzee!”
“Utayaweza masharti?” aliniuliza.
“Nitayaweza tu!”
“Ninapokuuliza nina maana yangu kwa sababu wapo wageni waliofika hapa wakihitaji utajiri kama unavyotaka wewe lakini baada ya kuwapa masharti ya dawa zangu walitoweka hawakurudi tena, je wewe utayaweza?” mganga aliniuliza.
“Shaka ondoa, nitayaweza mzee wangu,” nilimwambia.
Nilipomwambia hivyo, yule mganga aliniangalia na kuachia tabasamu kisha akasema:
“Kama utaweza nitafurahi sana kwani napenda mtu anayekuja hapa kutaka utajiri aupate.”
Alipotoa kauli hiyo alisimama na kuanza kuimba nyimbo ambazo sikuwa nikizielewa kabisa. Hakuishia kuimba tu bali akaanza kucheza pia. Nilibaki nikimwangalia, sikutaka kuzungumza kitu chochote kile kwani hata nguvu ya kufanya hivyo sikuwa nayo.
Akanisogelea na kunipaka unga fulani machoni mwangu. Ulikuwa na rangi nyeusi, alipoyapaka macho yangu, nikaanza kuhisi hali ya tofauti moyoni mwangu, furaha kubwa ambayo sikuwahi kuipata maisha yangu yote.
“Unajisikiaje?” aliniuliza.
“Najisikia vizuri….”
“Unahitaji utajiri wa aina gani? Wa kuku na mahindi au wa milele?” aliniuliza swali ambalo sikuwa nikilijua kabisa.
“Sijajua upo vipi!”
Mzee Mudi ndiye akachukua nafasi hiyo na kuanza kuniambia tofauti ya utajiri alioniambia mzee huyo; “Utajiri wa kuku ulikuwa ni kwamba kuku anatupiwa mahindi chini, anaanza kula, kama akila mahindi matano, basi utajiri wako utakuwa ni wa miaka mitano, kama akila mahindi ishirini, basi utajiri wako utakuwa wa miaka ishirini, baada ya hapo unafilisika na kufa,” mzee Mudi aliniambia.
“Hapana huo siupendi!” nilimwambia mzee Mudi.
“Kwa nini? Huo ndiyo mzuri!”
“Mimi nautaka huo mwingine.”
“Unaujua upo vipi?”
“Sijui, ila nautaka huohuo!” nilimwambia.
Utajiri niliosema kwamba niliutaka ulikuwa ni wa masharti makubwa. Niliambiwa hilo lakini nikasema kwamba nautaka huohuo na kama ni masharti nitayafanya yote lakini si kukubali ule wa mwanzo wa kuwa tajiri kwa kipindi fulani kisha kufa.
“Huu una masharti makubwa mawili,” aliniambia mganga.
“Yapi?”
“Moja, unatakiwa kuwaua wazazi wako wote,” aliniambia huku akikishika kitunguri kidogo kilichokuwa pembeni yake.
“Kuwaua wazazi wangu?”
“Ndiyo!”
“Na sharti jingine?” niliuliza huku nikionekana kuchanganyikiwa.
“Kufanya mapenzi na maiti ishirini,” aliniambia.
Kwanza nikashtuka, sikuonekana kuamini alichoniambia, nikamuuliza mara mbilimbili alisemaje, yeye akaniambia vilevile kwamba nilitakiwa kufanya mapenzi na maiti ishirini kama nilitaka kuwa tajiri, hivyo nilitakiwa kuchagua.
“Umechagua nini?”
“Kati ya nini na nini?”
“Kuwaua wazazi wako au kufanya mapenzi na maiti ishirini?” alinijibu kwa kuniuliza swali.
“Bora nifanye mapenzi na maiti ishirini,” nilimwambia japokuwa niliogopa mno.
Alichokifanya mzee yule ni kuchukua unga mwingine na kunipaka usoni kisha kuniambia nitulie kwa muda. Nilitulia hapohapo, sijui nini kilitokea, ghafla, nikajikuta nikitokea katika hospitali moja kubwa hapa jijini Dar es Salaam, nilishangaa, nilijiuliza nilifikaje mahali hapo lakini sikuwa na jibu.
Kulikuwa na watu wengi waliokuwa wakiendelea na shughuli zao, wagonjwa waliokuwa wakiingia na kutoka. Ghafla, nikasikia sauti ya yule mzee ikiniambia kwamba nilitakiwa kwenda mochwari, sikujua ilikuwa wapi lakini nikajikuta nikijiongoza mpaka kufika katika mlango ambao uliandikwa MOCHWARI kwa nje.
“Subiri hapo mpaka usiku,” niliisikia sauti hiyo.
Nilifanya kama nilivyoambiwa, nikasubiri mahali hapo. Ilikuwa jioni kama saa kumi na moja hivi. Hakukuwa na mtu aliyeniona, wengi walinipita bila kunisalimia. Ilipofika saa moja usiku, nikasikia sauti ile ikiniambia niende ndani ya mochwari ile, maelekezo mengine angeniambia, nikafanya hivyo na kuanza kuingia humo ambapo kulikuwa na majeneza mengi yaliyokuwa na maiti. Nikaambiwa nisubiri. Nilipotahamaki, eti ilikuwa saa sita usiku. Nikabaki nikitetemeka tu.
Je, kiliendelea nini? Usikose kufuatia Jumanne ijayo.
Wewe kiboko kweli duh
duh!kweli umedhamiria kuwa tajiri.