Kifo cha Mama Banza, Simulizi Inasikitisha
Marehemu Ramadhan Masanja ‘Banza Stone’, Khadija Masanja
Imelda Mtema, Risasi
DAR ES SALAAM: Simulizi ya kifo cha mama mzazi wa mwanamuziki nyota, marehemu Ramadhan Masanja ‘Banza Stone’, Khadija Masanja kilichotokea juzi Jumatatu, inasikitisha, kwa vile aliamka asubuhi ya siku hiyo akiwa mzima na ndiye aliyepokea maiti ya mjukuu wake, Sozi aliyefariki dakika chache kabla yake.
Aliyekuwa staa wa muziki wa dansi nchini, marehemu Ramadhan Masanja ‘Banza Stone’ (enzi za uhai wake).
Kwa mujibu wa kaka mkubwa wa marehemu Banza, Jamel alisema mpwa wake Sozi alikuja kujiuguza nyumbani kwao Sinza Kijiweni kwani alikuwa akisumbuliwa na kifua na mama yake Banza ndiye aliyekuwa akimuuguza. Siku hiyo ya Jumatatu, mpwa huyo alizidiwa hivyo wao kuamua kumpeleka hospitali ya Palestina.
Lakini kabla hawajafika hospitalini, Sozi alifariki hivyo kuwafanya warejee na mwili wake nyumbani na ni mama yao ndiye aliyewapokea na kuagiza maiti ya mjukuu wake isitiriwe vizuri chumbani.
“Baada ya muda mfupi kuna kitu tulitaka kumuuliza mama, lakini alikuwa ameenda chumbani kwake, tulipomuita na kuona kimya tukaenda chumbani kwake na kumkuta akiwa amelala na tulipojaribu kumchunguza tukagundua amefariki,” alisema Jamel.
“Yaani siwezi kuzungumza jinsi tulivyopatwa na mshtuko mkubwa sana, kwa maana tumeumia mno na hatukutarajia hicho kilichotokea kabisa baada ya kumkuta mama hapumui tena, ni maumivu makali” alisema kaka huyo huku akifuta machozi.
Mama wa mwanamuziki huyo na mjukuu wake walitarajiwa kuzikwa jana katika makaburi ya Sinza, jijini Dar.
Jamani mitihani hii mmh!