×

Hatari inayomkabili mwenye mapenzi kupita kiasi

smiling-couple_0620131146361
Kupenda ni jambo muhimu katika maisha ya mwanadamu, kwa sababu asilimia kubwa ya matendo ya mtu huongozwa na mapenzi. Miongoni mwetu kuna watu wanapenda waume/wake zao, mali, watoto, magari, vyakula, vinywaji, michezo na pengine aina fulani ya maisha.

Baadhi yetu tuko tayari kupoteza maisha kama tutaachwa na wapenzi au kukosa mambo tuliyoyapenda. Pamoja na kwamba moyo hupata maumivu pale mazuri yanapokosekana, bado kuna ukweli juu ya madhara ya kujitakia yanayoweza kuepukwa na mtu anayeumia kwa kiwango cha kukosa usingizi.

happy-couple-watching-tv-bedroomKupenda kwa kiwango cha kushindwa kujizuia  kuvumilia ni hatari kwa afya ya mwanadamu,  kwani uchunguzi unaonesha kuwa watu wengi wanaosumbuliwa na ugonjwa wa vidonda vya tumbo, moyo na wale wenye magonjwa yasiyoonekana kitaalamu pamoja na wanaokufa ghafla ni athari za msongo wa mawazo utokanao na kukosa mazuri wanayohitaji katika maisha yao.(Jiulize ni kipi kinachokutia simanzi moyoni mwako).

Kisaikolojia kuutesa moyo kwa sababu mpenzi wako kakukataa ni matokeo ya kufikiri vibaya kwani ushahidi uliopo miongoni mwetu unaonesha kuwa mapenzi si kitu cha kudumu kwa miaka mingi na anayesema anaweza kupenda jambo moja milele kwa kiwango kilekile ni mtu anayejiwekea mtego utakaomnasa mwenyewe na kumtesa.

Watu wengi tunaowaona wakipagawa baada ya kuachana na wenza wao au kuondolewa mambo fulani waliyokuwa wanayapenda ni wale walioyachukulia mapenzi kama kitu cha kudumu kisichoweza kubadilika, huku wakisahau ukweli kuwa wanayopenda kwa wakati huo hawakuzaliwa nayo na wala hawakuyapenda kabla. Nani alizaliwa anapenda kitu fulani na amedumu nacho hadi leo?

Licha ya kuwepo kwa umuhimu wa kujiaminisha katika kupenda kwa msingi wa muda mrefu, mtu hatakiwi kukataa mabadiliko yanapotokea kwani ni wazi kwamba tuliyopenda kuna siku yatatupa kisogo. Naam, wazazi, watoto na jamaa tunaowapenda kuna siku hatutakuwa nao maishani; tutafanyaje?

Hivyo ni jukumu la kila mtu anayetaka kuwa salama na maumivu ya moyo ya kumkosa ampendaye kuwa tayari kubadilika kutoka kupenda kitu cha awali mpaka kijacho, kuliko kung’ang’ania wazo moja na kujitesa nalo.

Historia ya mafanikio ya watu inaonesha kuwa waliokuwa tayari kuacha walivyovipenda na kuanza mambo mapya ndiyo waliofanikiwa. Wapo waliokulia katika mapenzi ya familia lakini walilazimika kuondoka na kwenda mahali fulani mbali kutafuta maisha yao, huko ndiko kukubali kuacha mapenzi ya awali na kutafuta mapya.

Katika hali ya kawaida ni vigumu sana kuondoka miongoni mwa watu uliowazoea, kuacha makazi yako na kuhamia mkoa mwingine, kuachana na mpenzi wako mliyeahidiana mambo mengi, lakini mafanikio na usalama wa maisha unataka mtu awe jasiri wa kupokea changamoto zinazohusu mapenzi.

Msomaji wangu, unaumia kwa sababu mpenzi wako ameamua kuachana na wewe na sasa unafikiria kujiua, hebu kaa chini ufikirie kabla ya kuwa na huyo maisha yako yalikuwa hayaendi? Jibu unalo wewe!

Tambua kuwa, dunia ina vitu vingi sana vya kupenda ambavyo vimeumbwa kwa ajili ya mwanadamu, usipopenda hiki haina maana hakuna cha kukufaa kipo na asipokupenda ndugu yako wapo marafiki watakaochukua nafasi ya mapenzi moyoni mwako na maisha yatasonga mbele kwa mafanikio makubwa, unachotakiwa ni kujiamini.

Ninaposema haya nisitafsiriwe vibaya kuwa nashawishi watu wasipende au wasipendane daima, hapana ninachojaribu kueleza hapa ni kuwa tayari kuyafanyia mabadiliko mapenzi yanayoonekana kutotimiza haja ya moyo.

Kupenda kitu kilekile kunahitaji maboresho, nitakuwa mtu wa mwisho kuamini kama mtu anaweza kupenda kitu cha aina ileile maisha yake yote na akahisi kutosheka.

Nadokeza tu; hata dunia tunayopenda kuishi inabadilika; ilivyokuwa miaka 30 iliyopita sivyo ilivyo leo.

Si ajabu hata sisi tumebadilika, tulikuwa vijana sasa ni wazee, tulikuwa wembamba leo ni wanene, kuna watu wamebadilisha upendo kutoka hali zetu za mwanzo mpaka hizi tulizonazo! TUJIAMINI.

Leave a Comment