
Mgombea wa nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameahidi kuendelea kuwajengea uwezo wavuvi wa Mkoa wa Kagera ili kufanya uvuvi wa kisasa kwa kuwapatia mafunzo, mikopo ya mitaji, na vyombo vya uvuvi vitakavyowawezesha kwenda mbali zaidi majini na kuongeza tija katika shughuli zao.
Aidha, kutokana na changamoto ya upungufu wa samaki katika maziwa mbalimbali, Dkt. Samia ameahidi kuwa, ikiwa atapewa ridhaa ya kuunda serikali, atawezesha pia vijana kuingia katika ufugaji wa samaki kwa kutumia vizimba, lengo likiwa ni kukuza uzalishaji na kuongeza tija kwa wavuvi wa mkoa wa Kagera na maeneo mengine nchini katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

Dkt. Samia alitoa ahadi hizo Alhamisi, Oktoba 16, 2025, wakati akizungumza na maelfu ya wananchi wa Bukoba Mjini, mkoani Kagera, katika Viwanja vya Kaitaba, ambako pia alisisitiza dhamira yake ya kuongeza thamani ya mazao ya mifugo kupitia kampeni ya ruzuku ya chanjo na utambuzi wa mifugo, ili kuhakikisha yanakidhi viwango na ithibati za kimataifa.
Katika hatua nyingine, mgombea huyo wa urais ameahidi kusaidia ujenzi wa machinjio za kisasa zitakazotoa huduma bora na zinazozingatia viwango vya kimataifa, ili kuwezesha bidhaa za mifugo na mifugo hai kuuzwa kwenye soko la dunia, akisema kuwa mahitaji ya bidhaa hizo ni makubwa kimataifa.
🔴 Tufuatilie kupitia YouTube ya Global TV, like, comment ili kuendelea kuhabarika kila siku kwa habari mbalimbali zenye ukweli na uhakika.