
Zohran Mamdani, mwenye umri wa miaka 34, amechaguliwa kuwa Meya mpya wa Jiji la New York, na kwa mara ya kwanza historia, Meya wa kwanza Muislamu wa jiji kubwa zaidi nchini Marekani.
Ushindi huu umekuja baada ya uchaguzi kukamilika, na Mamdani, anayejitambulisha kama msoshalisti wa kidemokrasia, kuibuka mshindi licha ya kuwa hajulikani sana miezi michache iliyopita. Kampeni zake zimejikita katika sera za kijamii, ikiwa ni pamoja na kutoza kodi zaidi kwa mamilionea ili kufadhili mipango mipya ya kijamii.
Katika sherehe za kusherehekea ushindi huo, Meya mteule Mamdani alionekana akipunga mikono na kutabasamu huku umati mkubwa ukiikabidhi kwa shangwe sauti yake: “Zohran! Zohran!”
Akizungumza na wafuasi wake, Mamdani alisema, “Leo inaashiria mwanzo wa siku mpya yenye matumaini kwa binadamu wote. Kwa muda mrefu, wafanyakazi wa New York wameambiwa na matajiri na wenye ushawishi kwamba madaraka si yao. Lakini katika miezi kumi na miwili iliyopita, mmeonyesha ujasiri wa kutafuta kitu kikubwa zaidi. Usiku huu, kinyume na matarajio yote, tumekipata. Mustakabali uko mikononi mwetu.”
Hotuba yake ilizingatia maono ya Mamdani kwa jiji la New York, lakini pia hakusita kumkabili kwa ucheshi mkosoaji wake mkuu, Rais wa Marekani Donald Trump. “Donald Trump, najua unatazama,” alisema Mamdani, “Nina maneno manne kwako: ongeza sauti.” Umati ulilipuka kwa shangwe kubwa. Mamdani aliongeza: “Ili umfikie yeyote kati yetu, italazimu upitie kwetu sote.”
Wakati huo, Trump aliandika katika ukurasa wake wa Truth Social: “… NA HIVYO NDIVYO INAVYOANZA!” Rais Trump alikuwa ametishia kukata ufadhili wa serikali kuu kwa Jiji la New York iwapo Mamdani angeshinda dhidi ya wagombea wa Upinzani Andrew Cuomo (mwaniaji huru) na Curtis Sliwa (Republican).
Kwa upande mwingine, chama cha Democrat kinatarajiwa pia kushinda uchaguzi wa ugavana katika majimbo ya Virginia na New Jersey. Aidha, wapiga kura wa California wamepitisha uamuzi wa kubadilisha mipaka ya majimbo ya uchaguzi ili kuimarisha nafasi ya chama cha Democrat kuelekea uchaguzi wa mwaka huu.