
Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ambaye pia ni Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, amempongeza Mhitimu wa Shahada ya Awali ya Sheria, Bi. Mary Barney Isaac Laseko, kwa kuandika historia mpya kwa kupata Daraja la Kwanza (First Class) katika Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo Tanzania (The Law School of Tanzania) rekodi ambayo haijawahi kupatikana kwa miaka 32.
Bi. Mary Laseko, ambaye ni mhitimu wa Shahada ya Sheria kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, amevunja rekodi iliyokuwa ikishikiliwa kwa muda mrefu na Prof. Hamudi Majamba, mmoja wa maprofesa mahiri wa sheria nchini. Tangu kuanzishwa kwa Law School, ni wanafunzi wachache sana waliokaribia kupata alama za juu, jambo lililoifanya rekodi hiyo kuwa ngumu kuvunjika kwa miongo mitatu.

Akizungumza katika hafla ya mahafali ya tatu ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) yaliyofanyika Novemba 20, 2025, Dkt. Kikwete alimpongeza Bi. Laseko kwa kile alichokieleza kuwa ni “ubora, nidhamu ya hali ya juu, na uthibitisho wa uwezo wa mwanafunzi wa Kitanzania katika taaluma ngumu kama sheria.”
Dkt. Kikwete alisema mafanikio hayo sio tu fahari kwa UDSM, bali pia ni ishara ya kuimarika kwa ubora wa elimu ya sheria nchini, akisisitiza kuwa taifa linahitaji vijana wenye umahiri na uwezo mkubwa katika sekta ya sheria.
“Kwa miaka 32 hakuna mwanafunzi aliyepata Daraja la Kwanza Law School, lakini leo tumeshuhudia historia ikiandikwa na kijana wetu. Mary amefungua mlango na ameonyesha kinawezekana,” alisema Dkt. Kikwete.

Kwa upande wake, mzazi wa mhitimu, Bw. Barney Isaac Laseko, alieleza furaha yake na kusema juhudi za mwanawe zimekuwa safari ndefu yenye kujituma, nidhamu na maombi. Mama wa mhitimu naye aliweka wazi kuwa mafanikio haya yatakuwa motisha kwa mabinti wengi nchini wanaotamani kusomea sheria.
Awali, Bi. Mary Laseko alionyesha shukrani zake kwa wazazi, walimu, na uongozi wa vyuo vyote viwili UDSM na Law School—akisema kuwa mafanikio yake ni matokeo ya ushirikiano, maombi na bidii ya kazi. Pia aliwahimiza wanafunzi wengine kuamini kuwa rekodi yoyote inaweza kuvunjwa endapo kuna malengo na kujituma.
Kwa mafanikio hayo makubwa, UDSM, Law School na jamii kwa ujumla wamepokea habari hii kama sura mpya ya kihistoria katika elimu ya sheria nchini Tanzania.