×

Sitasahau Nilivyokumbana na Jini Mwanaume-4

ILIPOISHIA WIKIENDA 

“Ndiyo. Nilikuwa bafuni wakati unanipigia,” nikatoa uongo. 

“Nilifikiri umesahau.”

 “Hapana, sikusahau. Nilikuwa nikupigie nikitoka bafuni.”

 Mzungu akanyamaza kimya kidogo. Pakapita ukimya wa sekunde kadhaa kabla ya sauti yake kusikika tena.

 “Umeshafikiria tukutane wapi,” akaniuliza.

 Nikamtajia hoteli moja ya palepale Sinza lakini ilikuwa mbali kidogo na nyumba ninayoishi.

 “Unaweza kufika?” nikamuuliza.

 “Ninaweza,” akaniambia.

 Akanyamaza kidogo kisha akaniuliza.

 SASA ENDELEA…

 Tukutane saa ngapi?”

“Kama saa kumi jioni hivi.”

Ningeweza kukutana naye wakati wowote lakini niliona nimtajie tu muda huo ili aone sikuwa mtu rahisirahisi.

“Saa kumi nikukute mimi au utanikuta wewe?” akaniuliza baada ya kimya kifupi.

“Vyovyote itakavyokuwa. Kama utawahi wewe kufika utanisubiri. Kama nitawahi mimi nitakusubiri.”

 “Ahadi za kizungu nitaziweza wapi?” Nilikuwa nikijisemea kimoyomoyo baada ya kuniuliza: “Nikukute mimi au utanikuta wewe?”

“Oke, hiyo ni ahadi nyingine itimize tafadhali.”

“Usijali Mr Smith.”

Nilipotaja jina lake akafurahi.

 “Nitajali kama hutatimiza ahadi yako,” akaniambia huku akionesha furaha aliyokuwa nayo.

“Ondoa wasiwasi, nitafika.”

“Oke, asante sana.”

 “Asante.”

 Nikakata simu.

Nikaendelea kunywa chai yangu huku nikimfikiria mzungu huyo. Kwa jinsi nilivyokuwa nikizifahamu tabia za wanaume nilishatambua kuwa yule mzungu alikuwa akinitaka kimapenzi lakini alishindwa kuniambia wazi. Badala yake aliamua kuzungusha maneno kwa kuniambia anataka tuwe marafiki bila kufafanua urafiki huo ni wa aina gani.

Nilikuwa nimeshaweka msimamo kuwa endapo ataweka pesa mbele, nitakuwa tayari kuwa naye mradi tu tutumie kinga kwani sikuwa tayari kuzaa mtoto wa kizungu.

Nikakumbuka kwamba aliwahi kuniuliza kama nilikuwa na mchumba. Nikajiambia kama atataka kuwa na uchumba na mimi itabidi kwanza nimchunguze tabia zake kabla ya kumkubalia.

Baada ya kumaliza kunywa chai niliondoa vyombo nikaenda kuviosha kisha nikarudi sebuleni kwangu na kupumzika kidogo huku nikichezea simu yangu.

 Saa sita mchana nikawa kwenye saluni moja kutengeneza nywele zangu. Nilitaka nikikutana na yule mzungu anione niko moto!

 Ilikuwa saa tisa nilipotoka saluni nikakodi bodaboda iliyonirudisha nyumbani. Nilibadili nguo nyingine kisha nikatoka. Wakati bodaboda inanishusha pale hotelini ilikuwa saa kumi kasoro dakika mbili hivi. Nilitaka niwahi ili yule mzungu aone niko makini.

 Wakati naingia kwenye lango la hoteli, kwa pembeni mwa macho yangu nilimuona mzungu huyo amesimama kando ya mti uliokuwa pembeni mwa ile hoteli.

 Sikugeuza uso wangu kumtazama. Nilijifanya kama sikumuona. Nilihisi kwamba alifika mapema akisubiri saa kumi ya ahadi yetu aingie ndani.

 Hata baada ya mimi kuingia  hotelini na kuketi, yule mzungu hakunifuata japokuwa alishaniona wakati ninashushwa na wakati ninaingia.

 Alisubiri mpaka ilipofika saa kumi kamili ndipo nilipomuona akiingia. Tabia yake ile ikanishangaza. Nikajiuliza ndiyo tabia za wazungu au?

 Wakati nawaza hivyo yule mzungu alikuwa akitupatupa macho kwenye ukumbi ule wa hoteli, akaniona.

 Akatembea taratibu kuelekea katika meza niliyokuwa nimeketi.

 “Oh karibu,” nikamwambia mara tu alipofika karibu na meza yangu.

“Asante.”

Alivuta kiti akaketi.

“Habari ya kutoka muda ule?” akaniuliza.

 “Nzuri. Ndiyo unafika?” nikajidai kumuuliza.

“Ndiyo ninafika,” akanijibu. Nikajua anasema uongo kwani nilishajua kuwa alifika mapema.

 “Asante kwa kutimiza ahadi yako,” akaniambia.

 Mhudumu naye alikuwa ameshafika.

 “Naweza kuwahudumia,” akatuambia.

Nikamtazama yule mzungu.

“Utakunywa nini?” akaniuliza.

 “Nitakunywa soda tu.”

“Hapana. Utakunywa bia. Sema unataka bia gani?”

 Nikacheka kidogo kabla ya kumuuliza:

 “Wewe unataka ninywe bia?”

“Ndiyo.”

“Haya niagizie.”

Mzungu akaagiza mzinga wa pombe kali mimi akaniagizia pombe ya kawaida.

 Mhudumu alipoondoka, mzungu huyo aliniambia alikuwa amefurahi kuwa na mimi siku ile. Alinitajia sehemu mbalimbali ambazo alisema aliwahi kuniona kabla ya siku ile na akanipenda.

 Sehemu alizonitajia ilikuwa ni kweli niliwahi kufika. Hapo nikajua kuwa kukutana kwetu hakukuwa kwa bahati tu bali alikuwa akinifuatilia.

 Mazungumzo yetu hayo yalikatizwa wakati yule mhudumu alipotuletea vinywaji tulivyoagiza.

Je, nini kiliendelea? Usikose kufuatilia kwenye Gazeti la Ijumaa Wikienda siku ya Jumatatu.  

Simulizi yangu ya “NILIVYOGEUZWA PAKA” sasa imetoka kwenye kitabu. Kwa mawasiliano ya kupata kitabu hicho piga namba 0712 777737. Kwa wasomaji wa Tanga wapige namba 0655 340572.

Leave a Comment