The House of Favourite Newspapers
gunners X

Mabasi 30 Ya Udart Kurejea Barabarani, Huduma Kufika Mloganzila – Prof. Shemdoe

0

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Prof. Riziki Shemdoe amefanya ziara ya ukaguzi katika karakana ya UDART eneo la Ubungo Jijini Dar es Salaam, ili kujionea hatua za ukarabati wa mabasi yaendayo haraka yaliyokuwa yamepata hitilafu.

Katika ziara hiyo Januari 06, 2026 Prof. Shemdoe amesema, Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan, ilitoa Shilingi Bilioni 1.2 kwa ajili ya kununua vipuri muhimu ikiwemo injini ili kufufua mabasi yaliyokuwa yamesitisha huduma.

Prof. Shemdoe amesema kupitia fedha hizo, jumla ya mabasi 30 yanatarajiwa kurejea barabarani, ambapo tayari mabasi 17 yamekamilika na yako tayari kuanza kutoa huduma kwa wananchi.

“Serikali iliona ni muhimu kuyarejesha mabasi haya barabarani. Ndio maana ilitoa fedha kwa ajili ununuzi wa vipuri na injini, na kati ya mabasi 30 tunayotarajia kuyarejesha, tayari 17 yamekamilika na yako tayari kuanza kazi,” amefafanua Prof. Shemdoe.

Aidha, Waziri Shemdoe amemuagiza Mkurugenzi wa UDART Bw. Pius Ngindo, kuhakikisha kuwa kuanzia kesho mabasi yaendayo haraka yaanze kufika Hospitali ya Mloganzila, ili kupunguza usumbufu kwa wananchi na wagonjwa wanaofuata huduma za matibabu katika hospitali hiyo.

Prof. Shemdoe ameahidi kuwa, Serikali itaendelea kuimarisha miundombinu ya usafiri wa umma ili kuhakikisha wananchi wanapata tabasamu kupitia huduma ya usafiri wa uhakika, salama na nafuu.

Leave A Reply