Waziri Kikwete Amtembelea Mama Maria Nyerere Na Mama Anna Mkapa

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Ridhiwani Kikwete amewatembelea na kuwajulia hali Mama Maria Nyerere, mke wa Hayati Baba wa Taifa na Rais wa kwanza wa Tanzania Mwalimu Julius Kambarage Nyerere nyumbani kwake Msasani jijini Dar es Salaam na Mama Anna Mkapa, mke wa Hayati Benjamin William Mkapa nyumbani kwake Masaki Jijini Dar es Salaam Januari 06, 2026.
Kikwete amesema, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan anathamini sana mchango wa Viongozi Wakuu wa Kitaifa waliomtangulia na ataendelea kusimamia na kutunza familia hizo kwa mujibu wa Katiba na Sheria zilizowekwa.

Aidha, Ridhiwani amesema, kuwatembelea na kuwajulia hali wake hao wa Viongozi Wastaafu ni moja ya majukumu yake ambayo anayatekeleza kwa lengo la kuwajulia hali, kusikiliza changamoto zilizopo na kuzitafutia ufumbuzi kwa mujibu wa Katiba na Sheria zilizowekwa.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Juma Mkomi amesema ofisi hiyo itafanyia kazi maoni na ushauri uliotolewa na wajane hao.
Aidha, Mama Maria Nyerere amemshukuru Kikwete kwa kupata nafasi ya kumtembelea na kumjulia hali na amempongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuijali familia yake wakati wote pasipo kuchoka.
Naye, Mama Anna Mkapa ameishukuru ofisi hiyo kwa kufuatilia kwa karibu masuala yanayowahusu na kuyatafutia ufumbuzi.



