
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM- TAMISEMI), anayeshughulikia afya Dkt. Jafar Seif, amesema Serikali imefanya tathmini na kuainisha vituo vya afya kongwe 532 kote nchini ambavyo vinahitaji kuongezewa miundombinu na kukarabatiwa.
Dkt. Seif ameyesema hayo Februari 2, 2026 katika kipindi cha maswali na majibu Bungeni jijini Dodoma, wakati akijibu swali la Saashisha Mafuwe Mbunge wa Jimbo la Hai mkoani Kilimanjaro aliyetaka kujua ni lini Serikali itakarabati Kituo cha Afya cha Masama pamoja na nyumba za watumishi.
Katika majibu yake Dkt. Seif amesema jumla ya Shilingi Bilioni 102.08 zinahitajika kwa ajili ya kutekeleza uboreshaji wa vituo hivyo, ambapo Serikali itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya ukarabati wa vituo vya afya kongwe kote nchini kikiwemo kituo cha afya Masama.
Kadhalika akijibu maswali ya nyongeza ya baadhi ya Wabunge Dkt. Seif amesema Serikali tayari imetenga zaidi ya Shilingi Bilioni 30 kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya vya kimkakati katika Majimbo 120 na tayari Wizara imeomba fedha kwa ajili ya majimbo mengine 94 ambayo yote yataingia katika mpango huo ili kuwezesha ujenzi wa vituo vipya vya afya vya kimkakati kuanza katika maeneo mbalimbali.