Rais Samia Atangaza Fursa za Uwekezaji Tanzania Mbele ya Viongozi wa Dunia

Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ametoa hakikisho la miundombinu bora ya uwekezaji nchini kwa wawekezaji duniani, akisema Tanzania imewekeza vema katika ujenzi wa reli, nishati, bandari na miundombinu ya uchukuzi.
Miundombinu mingine aliyosema imewekezwa nchini ni kutengwa kwa maeneo maalumu ya uwekezaji na dirisha moja la uwekezaji, yote hayo yamefanywa ili kujenga mazingira rafiki kwa wawekezaji wa muda mrefu.

Dkt Samia ameyasema hayo usiku wa kuamkia leo, Jumatano Februari 4, 2026 alipozungumza katika uzinduzi wa Jukwaa la Uwekezaji Duniani kwa upande wa Afrika (GAIS), linalofanyika Dubai, katika Taifa la Falme za Kiarabu.
Amesisitiza wawekezaji hawatafuti fursa pekee, bali uaminifu uthabiti wa sera, taasisi imara na Serikali zinazotekeleza ahadi zake, akidokeza Tanzania ina sifa zote hizo.
Ushiriki wa Tanzania katika GAIS unaakisi dhamira ya nchi ya kwenda kwenye ushirikiano uliopangiliwa vema na unaoendana na vipaumbele vya maendeleo ya taifa na matarajio ya wawekezaji wa kimataifa.

