×

Fedha za Majini Zilivyoniendesha Puta

ILIPOISHIA

Baada ya hapo nikatoka nje. Muda huo baadhi ya watu walikuwa wanakwenda mashambani na wanawake walikuwa wakifanya usafi nje ya nyumba zao.
Watu wa kwanza kuwaarifu walikuwa ni wale majirani zetu wa karibu. Baada ya kuwapa taarifa na wakafika nyumbani kwangu. Kuna waliojitolea kusambaza habari zile kwa majirani wa mbali zaidi.

SASA ENDELEA
Ndugu wa upande wa baba walipofika tulikubaliana kuwa marehemu tumzike mchana wa siku ileile kwa vile hakukuwa na cha kungoja.

Tuliita walimu waliokuja kuuandaa mwili wa marehemu kwa ajili ya mazishi ikiwa ni pamoja na kufanya visomo vilivyohitajika. Hadi inafika saa sita mchana, kila kitu kikawa tayari. Mwili wa marehemu ulitiwa kwenye jeneza na kutolewa kwa ajili ya kupelekwa msikitini kuswaliwa.
Baada ya marehemu kuswaliwa alitolewa kupelekwa makaburini tayari kwa ajili ya mazishi.
Tulipomaliza kuzika tulirudi nyumbani ambako baada ya kufanyika dua ya mwisho ya kumuombea marehemu, nilitoa hotuba fupi kuwashukuru ndugu jamaa na majirani walioshirikiana na mimi katika msiba huo.
Kama ilivyo kawaida katika mazishi yoyote yale, niliuliza kama marehemu alikuwa akimdai mtu yeyote au kama alikuwa anadaiwa na mtu yeyote yule.
Sikupata jibu. Nikatoa angalizo kama kutatokea mtu yeyote ambaye anadaiwa na marehemu au anamdai marehemu anifuate mimi na kunifahamisha anachodai ili niweze kumlipa na kama anadaiwa yeye anilipe.
Baada ya hapo niliwashukuru tena watu wote na kuwapa ruhusa ya kuondoka. Watu wakatawanyika na kurudi katika shughuli zao.

Tulibaki ndugu watupu tukaweka vikao vyetu. Baada ya vikao hivyo ndugu hao nao wakatawanyika. Nyumbani kulibaki wanawake wachache ambao walikaa kwa siku tatu kukamilisha mila zetu. Siku ile ya tatu walioga na kuondoka.
Nikabaki peke yangu kwenye nyumba ile. Mara tu baada ya watu kuondoka nilijifungia chumbani mwangu nikalitoa lile sanduku la pesa. Nililifungua nikatoa zile pesa na kuzimwaga kwenye godoro. Zilienea godoro lote.
Nikaanza tena kuzihesabu ili nijue zilikuwa ni kiasi gani. Siku ile ya kwanza nilipozihesabu niliziacha nusu. Sasa nikaamua kuzihesabu zote.

Kwa vile pesa zenyewe ziliwekwa katika vitita vya shilingi milioni moja moja. Ilinirahisishia kazi ya kuzihesabu.
Zile pesa nilizozihesabu nilikuwa ninazirudisha mle kwenye sanduku.
Nilianza kuhesabu kutoka saa tatu asubuhi, hadi inafika saa sita mchana sikuwa nimezimaliza pesa zote. Kulikuwa na kiasi kikubwa ambacho kilikuwa kimebaki.
Nikaendelea kuhesabu ili nikimalize kiasi hicho lakini kila nilivyoendelea niliona kama vile zile pesa zilikuwa haziishi. Nikaanza kupata wasiwasi.
Sanduku lilikuwa linakaribia kujaa lakini pesa zilizobaki zilikuwa nyingi kuliko zile nilizozihesabu na kuzitia kwenye sanduku.

“Pesa zote hizi si zilitoka kwenye sanduku hili hili?” nikawa najiuliza.
“Mbona sasa zinaonekana ni nyingi?” nikaendelea kujiuliza.
Ile kazi ya kuhesabu ikaanza kunitia uvivu. Sasa nikataka nizirudishe zile pesa zote kwenye sanduku nione kama zitajaa na kubaki.

Baada ya kufanya hivyo nikaona maajabu. Pesa hizo ambazo sikuwa nimezihesabu ambazo niliona zilikuwa nyingi kuliko zile nilizozitia kwenye sanduku, nilipozirudisha kwenye sanduku hilo ziliingia zote bila kubaki.
Kwa kweli nilipata wasiwasi. Nikazitazama pesa hizo kisha nikalifunga lile sanduku na kulirudisha mvunguni.
Nikakaa kitandani na kujiuliza, baba yangu alipata wapi pesa zile wakati mwenyewe alikuwa maskini.

Lakini kulikuwa na matukio ya wakati wa nyuma ambayo yalinifikirisha. Ile nyumba tuliyokuwa tunakaa pale kijijini ilikuwa ni ya gharama kubwa na aliijenga marehemu baba yangu. Hakukuwa na mtu yeyote ambaye alijua baba yangu alipata wapi pesa za kujengea nyumba ile wakati rasilimali yake ilikuwa ni shamba dogo tu.

Pia nilikumbuka kuwa aliwahi kufungua duka kubwa halafu akalifunga. Hakukuwa na aliyejua alipata wapi pesa za kufungulia duka lile. Pia alinunua gari la thamani akaliendesha kwa siku chache tu kisha akaliuza.
Wakati ule sikupata akili ya kumuuliza baba alipata wapi pesa za kufungua duka au kununua gari, nilipata akili ya kumuuliza kwa nini alilifunga lile duka na kwa nini aliuza lile gari.
Jibu lake lilikuwa alilifunga lile duka kwa sababu wachawi wakiona ana mali watamuandama sana. Na kuhusu gari aliniambia ameliuza kwa kuogopa fitina za watu.

Sasa niligundua kuwa baba yangu alikuwa na pesa lakini hakutaka kutambulika. Alihofia kwamba endapo angejulikana kuwa ni tajiri angeuawa kwa mujibu wa mtazamo wake.
Kwa vile hakutaka ajulikane kuwa alikuwa na pesa aliishi kama maskini. Na hata mimi mwanawe nilijua kuwa baba yangu alikuwa maskini. Lakini kumbe hakuwa hivyo.

Lakini kitu ambacho kiliumiza akili yangu kukifikiria ni jinsi baba yangu alivyopata pesa zile. Baba yangu hakuwa na rasilimali yoyote zaidi ya shamba, alipata wapi pesa hizo?
Wakati ninajiuliza swali hilo likanijia swali jingine, kwa nini pesa hizo zinaonekana kama zina miujiza fulani. Wakati wa kuzihesabu zinaonekana kuwa ni nyingi na huwezi kuzimaliza?
Labda swali hilo ndilo ambalo lilinipa utata zaidi kwa sababu lilikuwa halina jibu.

Baada ya kutopata jibu nilitoka mle chumbani nikaingia katika chumba cha marehemu baba yangu. Nilichutama chini ya kitanda nikatia mkono na kutoa ule mkoba ambao niliuona mvunguni.
Itaendelea wiki ijayo

Leave a Comment