
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Geita imewafikisha mahakamani Mbunge wa Jimbo la Chato Kaskazini, Cornel Magembe , na Mbunge wa Jimbo la Chato Kusini, Paschal Lutandula , pamoja na madiwani watatu wa Chato, akiwemo aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Bathromeo Manunga, wakituhumiwa kujihusisha na vitendo vya rushwa katika nyakati tofauti.
Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za TAKUKURU Mkoa wa Geita, Mkuu wa TAKUKURU mkoani humo, James Ruge, alisema Cornel Magembe kwa kushirikiana na Frank Francis, aliyekuwa Diwani wa Kata ya Mganza, wanatuhumiwa kukusanya madiwani wateule 20 wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato kwa lengo la kuwashawishi kwa kuwapa fedha, chakula na malazi ili wawapigie kura katika uchaguzi wa ndani wa Mwenyekiti wa Halmashauri.
Ruge alieleza kuwa tukio hilo linadaiwa kutokea kati ya tarehe 28 Novemba 2025 na tarehe 30 Novemba 2025, na kwamba uchunguzi wa TAKUKURU ulibaini kuwepo kwa viashiria vya vitendo vya rushwa, hali iliyopelekea watuhumiwa kufikishwa mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria.