×

Mwili wa Lukuvi Ulivyowasili Iringa kwa Shughuli za Mwisho – Picha

Mwili wa aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), William Lukuvi, umefikishwa katika Kiwanja cha Ndege cha Iringa Machi 29, 2026, kwa ajili ya kuendelea na shughuli za heshima za mwisho kabla ya mazishi yake.

Kwa mujibu wa ratiba, mwili wa marehemu Lukuvi unatarajiwa kuagwa rasmi Machi 30, 2026 katika Parokia ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, Kanisa Kuu la Kihesa, lililopo katika Jimbo Katoliki la Iringa. Shughuli hiyo ya kuaga itahusisha viongozi mbalimbali wa serikali, viongozi wa dini, ndugu, jamaa na wananchi kwa ujumla watakaofika kutoa heshima zao za mwisho.

Mwili huo ulisafirishwa kutoka jijini Dar es Salaam leo Machi 29, 2026, baada ya kuagwa rasmi katika Viwanja vya Karimjee tarehe 28 Machi, 2026, ambapo viongozi mbalimbali wa kitaifa walihudhuria kutoa salamu za mwisho na heshima zao.

Baada ya zoezi la kuaga kukamilika Iringa, mwili wa marehemu Lukuvi utasafirishwa kuelekea Kijiji cha Idodi kilichopo katika Wilaya ya Iringa Vijijini, ambapo maziko yake yatafanyika Machi 31, 2026.

William Lukuvi alifariki dunia tarehe 25 Machi, 2026 katika Hospitali ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma alipokuwa akipatiwa matibabu.

Shughuli zote za heshima za mwisho zinaendelea kufanyika kwa utaratibu maalum wa serikali, huku zikitarajiwa kuhudhuriwa na maelfu ya wananchi kutoka maeneo mbalimbali nchini wanaokuja kumuaga kiongozi huyo aliyewahi kuhudumu katika nyadhifa mbalimbali serikalini.

Leave a Comment