
Dar es Salaam, Aprili 1, 2026 — Kadiri mahitaji ya huduma za malipo ya kidijitali yanavyozidi kuongezeka nchini, Benki ya Exim Tanzania imeingia ubia wa kimkakati na The Voice TZ, eneo maarufu la burudani na huduma za chakula, kwa lengo la kurahisisha na kuimarisha matumizi ya malipo yasiyotumia fedha taslimu.
Ushirikiano huo unakuja wakati ambapo Watanzania wengi wanatafuta njia za malipo zilizo salama, za haraka na rahisi, hasa katika kipindi hiki kinachoelekea msimu wa sikukuu.
Kupitia makubaliano hayo, wateja wa The Voice TZ sasa wataweza kulipia huduma kwa kutumia kadi za Benki ya Exim au huduma ya Lipa ChapChap, hatua itakayopunguza utegemezi wa fedha taslimu na kuboresha uzoefu wa wateja.
Aidha, wateja watakaotumia kadi za Exim watanufaika na punguzo la asilimia 10 kwenye bili zao. Malipo yatathibitishwa papo hapo, huku marejesho yakifanyika mara moja endapo kutatokea hitilafu. Risiti zitatolewa kupitia ujumbe mfupi wa simu (SMS) au nakala ya karatasi.

Akizungumza kuhusu ushirikiano huo, Mkuu wa Huduma za Wateja Binafsi wa Benki ya Exim Tanzania, Andrew Lyimo, alisema hatua hiyo inalenga kuongeza urahisi na thamani kwa wateja.
“Katika kipindi cha sikukuu ambacho maeneo ya burudani hupokea wateja wengi, huduma hizi zitawawezesha wateja kufanya malipo kwa urahisi bila usumbufu wa kubeba fedha taslimu,” alisema Lyimo.
Benki hiyo imeeleza kuwa maboresho hayo ni sehemu ya mkakati wake wa muda mrefu wa kuhamasisha matumizi ya malipo ya kidijitali kupitia uwekezaji katika mifumo ya kisasa, huduma za kadi na suluhisho la Lipa ChapChap.
Kwa upande wake, Mkuu wa Masoko na Mawasiliano wa benki hiyo, Stanley Kafu, alisema benki inaendelea kuweka mteja katikati ya huduma zake.

“Wateja watanufaika na malipo ya haraka ya ‘tap and go’, marejesho ya papo hapo na uwazi wa gharama, jambo linalojenga imani katika matumizi ya huduma za kidijitali,” alisema Kafu.
Naye Mkurugenzi wa Masuala ya Kiufundi wa The Voice TZ, Deogratius Stephen, alisema ushirikiano huo utaongeza ubora wa huduma kwa wateja wao.
“Sasa wateja wetu wanaweza kulipa kwa haraka na kwa usalama, na hivyo kupata muda zaidi wa kufurahia huduma zetu,” alisema.
Mpango huo unatarajiwa kuongeza matumizi ya malipo ya kidijitali si tu katika The Voice TZ, bali pia katika maeneo mengine ya biashara na huduma nchini.
Hatua hiyo inaakisi jitihada za Benki ya Exim katika kuleta suluhisho za kisasa zinazolenga kuboresha huduma za kifedha na kurahisisha maisha ya Watanzania.
