
Huduma mpya ya kifedha kwa sekta ya afya imezinduliwa rasmi wakati wa Kongamano la Kitaifa la Wadau wa Sekta ya Afya binafsi linaloendelea jijini Dodoma, ambapo watoa huduma sasa wanaweza kupata mikopo kwa urahisi kupitia mfumo wa Lipa Namba.
Akizungumza katika kongamano hilo, Mkuu wa Kanda ya Kati wa Vodacom Tanzania Plc, Chiha Nchimbi, alieleza kuwa huduma hiyo ya “Afya Mkopo” inalenga kuwainua watoa huduma binafsi kwa kuwapatia mitaji ya haraka, nafuu na yenye masharti rafiki.

Huduma hiyo inatolewa kwa ushirikiano kati ya Vodacom Tanzania Plc, PharmAccess Foundation pamoja na Medical Credit Fund, ikiwa na lengo la kuboresha upatikanaji wa fedha kwa vituo vya afya binafsi nchini.
Naibu Waziri wa Afya, Florence Samizi, alipotembelea banda la Afya Mkopo, alipata maelezo ya kina kuhusu namna mfumo huo unavyofanya kazi, huku akisisitiza umuhimu wa ubunifu wa kifedha katika kuboresha huduma za afya nchini.
Kupitia mfumo wa Lipa Namba, watoa huduma wanaweza kupata mikopo kwa haraka zaidi, jambo linalotarajiwa kusaidia kupanua huduma, kuboresha miundombinu ya vituo vya afya na kukuza biashara zao kwa ujumla.

Viongozi wengine waliokuwepo katika tukio hilo ni pamoja na Dk. Heri Marwa, Mkurugenzi wa PharmAccess Foundation, pamoja na Maula Mafuru, Meneja Mauzo wa M-Pesa Kanda ya Kati, wakionesha mshikamano katika kuendeleza suluhisho za kifedha ndani ya sekta ya afya.
Mpango huu unaonekana kuwa hatua muhimu katika kuimarisha sekta binafsi ya afya kwa kutumia teknolojia ya kidijitali na huduma za kifedha jumuishi.
