
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimepatwa na pigo kutokana na kifo cha Aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa chama hicho, Anna Maulidah Komu, aliyefariki dunia Aprili 28,2026 majira ya saa tano usiku akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Lumumba visiwani Zanzibar.
Taarifa za kifo chake zimepokelewa kwa huzuni kwa miongoni mwa wanachama na viongozi wa chama hicho, waliomuelezea kama mwanasiasa aliyekuwa mstari wa mbele katika harakati za demokrasia na ushiriki wa wanawake katika siasa nchini.
Akizungumza na Nipashe Digital kuhusu msiba huo, Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA Zanzibar, Ali Ibrahim, amesema hadi mauti yanamkuta Anna alikuwa bado mwanachama hai wa chama hicho na aliendelea kushiriki katika shughuli mbalimbali za kisiasa na kijamii.
“Anna alikuwa na mchango mkubwa katika kukijenga chama kupitia nafasi mbalimbali za uongozi alizowahi kushika, na alikuwa mmoja wa wanawake waliothubutu kuingia katika siasa za ushindani kwa ujasiri mkubwa,” Ibrahim amesema.
Katika historia yake ya kisiasa, Anna aliwahi kugombea nafasi ya Makamu wa Rais kupitia CHADEMA katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2005 na pia aliwahi kuwa Mbunge wa Viti Maalum, akitetea masuala ya wanawake, vijana na maendeleo ya jamii.