×

Kitulo Marathon Yavutia Washiriki Wengi, Kuanza Rasmi kwa Mashindano

WASHIRIKI wa mbio za Kitulo Garden Marathon wameanza kujipasha moto mapema kabla ya kuanza rasmi kwa mashindano hayo yanayofanyika katika mazingira ya kipekee ya Hifadhi ya Kitulo, yakilenga kuhamasisha afya, utalii na burudani.

Akizungumza kabla ya kuanza kwa mbio hizo, mmoja wa waratibu Mony Luvanda, mbio ambazo zinasimamiwa na Kampuni ya Events and Promotions chini ya Mkurugenzi wake Dkt. Toba Nguvila, ambaye pia ni Katibu Tawala (RAS) Mkoa wa Arusha, amesema maandalizi ya awali ikiwemo mazoezi ya kunyoosha viungo ni muhimu ili kuhakikisha washiriki wanashiriki kwa usalama bila kupata majeraha.

Mashindano hayo yanajumuisha umbali wa kilometa tano (Fun Run), kilometa 10 pamoja na kilometa 21.1 (nusu marathon), ambapo washiriki wamehimizwa kushiriki kikamilifu bila kutoa visingizio.

Mbali na mashindano, tukio hilo pia limepambwa na vivutio vya utalii pamoja na burudani ikiwemo nyama choma na shughuli za kijamii zitakazoendelea hadi kesho asubuhi.

Kitulo Garden Marathon, inayofanyika chini ya kaulimbiu “Hifadhi Yetu, Fahari Yetu,” inalenga kuhamasisha utunzaji wa mazingira sambamba na kukuza utalii wa ndani.

Leave a Comment