
Msanii maarufu wa muziki na filamu, Selena Gomez, ameweka sokoni jumba lake la kifahari lililopo eneo la Los Angeles kwa thamani ya dola milioni 6.5 (zaidi ya shilingi bilioni 17 za Kitanzania).
Kwa mujibu wa taarifa, nyumba hiyo ipo Encino katika eneo la kifahari lenye ulinzi mkali, ikiwa na vyumba sita vya kulala, bafu 10 na ukubwa wa takribani futi za mraba 11,500.

Jumba hilo lina kila aina ya huduma za kisasa ikiwemo sebule kubwa, jiko la kisasa, chumba cha chakula (dining), pamoja na huduma za ziada zinazopatikana kwa mastaa wakubwa.
Miongoni mwa vivutio vilivyopo ndani ya nyumba hiyo ni:
- Chumba cha kuhifadhia mvinyo (wine cellar)
- Ukumbi wa kutazama filamu (media room)
- Chumba cha massage
- “Glam room” kwa maandalizi
- Gym binafsi
- Ofisi ya kazi
- Studio ndogo ya kurekodia sauti
Nje ya nyumba, eneo lake lina ukubwa wa karibu ekari moja, likiwa na maporomoko ya maji, kijito kinachoingia kwenye bwawa la kuogelea pamoja na spa.

Hatua ya kuuza nyumba hiyo inakuja baada ya Gomez kuhamia kwenye jumba jingine kubwa zaidi pamoja na mpenzi wake, Benny Blanco, huko Beverly Hills, walilonunua kwa dola milioni 35 mwaka uliopita.
Nyumba hiyo pia ina historia ya kipekee kwani awali iliwahi kumilikiwa na mwanamuziki marehemu Tom Petty.
Kwa sasa, jumba hilo limewekwa sokoni rasmi na mawakala wa mali isiyohamishika, likisubiri mnunuzi mwenye uwezo wa kumudu gharama hiyo kubwa.