
Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Pwani, Boniface Jacob ‘Boni Yai’, amesema kuwa uwepo wa Chadema ni muhimu katika kuhakikisha wananchi wanapata sauti ya kuwasemea na kutetea maslahi yao katika masuala mbalimbali ya kitaifa.
Akihutubia mamia ya wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Mei 8, 2026 jijini Arusha, Jacob alisema kufungiwa kwa shughuli za chama hicho kwa kipindi cha mwaka mmoja kulisababisha wananchi wengi kubaki bila jukwaa la kueleza changamoto zao.
Kwa mujibu wa Jacob, kipindi hicho kilionyesha namna ambavyo wananchi walivyokuwa wanakosa sauti ya kuibua masuala yanayowagusa moja kwa moja katika maisha yao ya kila siku.
“Sisi Chadema tulifungiwa kwa mwaka mmoja, na ndani ya kipindi hicho hakuna mtu aliyeona cheche, kwa sababu msemaji rasmi wa wananchi anayezungumzia shida za Watanzania ni Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),” alisema Jacob.
Katika hotuba yake, Jacob pia aliwahimiza wananchi kuendelea kushiriki katika masuala ya kisiasa na kutetea haki zao kwa njia za kisheria na kidemokrasia.