
Tehran — Iran imetoa onyo kali ikisema inaweza kuongeza kiwango cha urutubishaji wa urani hadi asilimia 90 iwapo itashambuliwa tena, hatua inayoweza kuzidisha kwa kiasi kikubwa mvutano uliopo katika eneo la Mashariki ya Kati.
Kauli hiyo imetolewa na msemaji wa kamati ya usalama wa taifa ya bunge la Iran, Ebrahim Rezaei, ambaye amesema suala hilo linaweza kuwasilishwa rasmi bungeni kwa ajili ya kujadiliwa na kuamua hatua zinazofuata.
Kwa mujibu wa wataalamu wa masuala ya nyuklia, kiwango cha urutubishaji wa urani cha asilimia 90 kinahesabiwa kuwa karibu na kile kinachotumika kutengeneza silaha za nyuklia. Hivi sasa, Iran inadaiwa kufikia kiwango cha takriban asilimia 60, hatua ambayo tayari imeibua wasiwasi mkubwa kimataifa.
Onyo hilo linakuja wakati ambapo mvutano kati ya Iran na Marekani ukiendelea, kufuatia kauli ya Rais Donald Trump kwamba makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya pande hizo mbili yako katika hali tete.
Hali hiyo pia inaendelea kuchochewa na historia ya mashambulizi yaliyowahi kulenga vituo vya nyuklia vya Iran, yaliyofanywa na Marekani na Israel mwaka jana. Hata hivyo, bado kuna sintofahamu kuhusu kiasi cha urani yenye kiwango cha juu kilichosalia nchini humo baada ya mashambulizi hayo.
Mashirika ya ujasusi ya Marekani yanaendelea kuonya kwamba mpango wa nyuklia wa Iran unaweza kuwa tishio la usalama wa kimataifa iwapo akiba ya urani haitadhibitiwa au kuondolewa.