Mkurugenzi Mtendaji na Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB Bank Plc, Ruth Zaipuna, anatarajiwa kuiwakilisha Tanzania na sekta ya benki ya Afrika katika mkutano wa kimataifa wa biashara wa Cambridge Africa Business Conference 2026 utakaofanyika Mei 30, 2026 katika Cambridge Judge Business School chini ya University of Cambridge.
Ushiriki wa Zaipuna katika mkutano huo unaonekana kuwa hatua muhimu kwa sekta ya fedha nchini pamoja na kuonesha namna taasisi zinazoongozwa na Waafrika zinavyozidi kupata nafasi katika majukwaa ya kimataifa ya biashara na uwekezaji.
NMB Kuelezea Safari ya Mageuzi
Katika mkutano huo, Ruth Zaipuna anatarajiwa kutoa hotuba kuu itakayolenga kuelezea safari ya mageuzi ya NMB na mchango wake katika kukuza uchumi wa Tanzania.
Hotuba hiyo itaangazia namna NMB ilivyokua kutoka katika misingi ya huduma ndogo za kifedha hadi kuwa moja ya taasisi kubwa na zenye ushawishi mkubwa katika sekta ya benki nchini Tanzania.
Aidha, anatarajiwa kuelezea mchango wa benki hiyo katika kukuza ujumuishaji wa kifedha, kusaidia biashara ndogo na za kati pamoja na kuimarisha huduma za kidigitali zinazorahisisha upatikanaji wa huduma za kifedha kwa Watanzania.
Afrika Kujadili Mitaji, Ubunifu na Ukuaji
Mkutano huo wa mwaka 2026 umebeba kaulimbiu ya “Building Africa’s Future: Capital, Innovation and Continental Growth” ikiwa na lengo la kujadili nafasi ya Afrika katika kuchochea maendeleo kupitia mitaji, ubunifu na uwezo wa taasisi za Kiafrika kufanya kazi kwa kiwango cha bara.
Majadiliano pia yanatarajiwa kugusia nafasi ya African Continental Free Trade Area (AfCFTA) katika kufungua fursa mpya za biashara, uwekezaji na ukuaji wa uchumi katika nchi mbalimbali za Afrika.
Ruth Zaipuna: Ni Heshima kwa NMB na Tanzania
Akizungumzia mwaliko huo, Ruth Zaipuna alisema kuwa ushiriki wake katika mkutano huo ni heshima kubwa kwa NMB pamoja na Tanzania kwa ujumla.
Alisema safari ya NMB inaonesha kuwa taasisi zinazoongozwa na Waafrika zina uwezo wa kujenga ubora wa kiwango cha kimataifa huku zikiendelea kuwa karibu na mahitaji ya wananchi, wafanyabiashara na vipaumbele vya maendeleo ya taifa.
Zaipuna pia alisisitiza umuhimu wa taasisi za kifedha za Afrika kuendelea kuwekeza katika ubunifu, teknolojia na huduma zinazogusa maisha ya wananchi ili kuharakisha maendeleo ya kiuchumi katika bara hili.
