Trump Aondoka na Mabosi 17 wa Kampuni Kubwa za Marekani Kuelekea China
Global Publishers May 13, 2026 0 Comments
SHARE THIS:
Rais wa Marekani Donald Trump ameambatana na viongozi wakuu wa kampuni kubwa duniani katika ziara yake rasmi nchini China wiki hii, huku lengo kuu likiwa kuimarisha mahusiano ya kiuchumi na kiteknolojia kati ya mataifa hayo mawili yenye ushindani mkubwa duniani.
Miongoni mwa viongozi hao ni Mkurugenzi Mtendaji wa Apple, Tim Cook, Elon Musk wa Tesla na SpaceX, pamoja na Larry Fink wa BlackRock. Wengine ni viongozi kutoka Meta, Visa, Boeing, JPMorgan, Goldman Sachs, Mastercard, Citi na makampuni mengine makubwa ya Marekani.
Kwa mujibu wa taarifa, jumla ya viongozi 17 wa kampuni za Marekani wamejiunga na ujumbe rasmi wa Trump kuelekea Beijing kwa ajili ya mkutano na Rais wa China Xi Jinping.
Ziara hiyo inatajwa kuwa muhimu wakati ambapo Marekani na China zinaendelea kushindana katika masuala ya biashara, teknolojia ya akili bandia (AI), pamoja na uzalishaji wa semiconductor na chip za kisasa za kompyuta.
Miongoni mwa viongozi wengine waliopo katika ujumbe huo ni:
Dina Powell McCormick wa Meta
Kelly Ortberg wa Boeing
Ryan McInerney wa Visa
Stephen Schwarzman wa Blackstone
Jane Fraser wa Citi
David Solomon wa Goldman Sachs
Michael Miebach wa Mastercard
Jacob Thaysen wa Illumina
Awali, Mkurugenzi wa Nvidia Jensen Huang hakuwa kwenye orodha ya wajumbe hao, jambo lililozua mshangao kutokana na nafasi kubwa ya kampuni yake katika ushindani wa teknolojia ya AI kati ya Marekani na China. Hata hivyo, baadaye Huang alionekana akipanda ndege ya Air Force One kuelekea Beijing baada ya ndege hiyo kusimama Anchorage, Alaska.
Msemaji wa Nvidia alisema Huang amealikwa na Rais Trump ili kusaidia malengo ya Marekani katika mkutano huo.
Pia, uwepo wa Sanjay Mehrotra, Mkurugenzi wa Micron Technology, umeonekana kuwa wa muhimu baada ya China kuweka vikwazo kwa baadhi ya chip za kampuni hiyo mwaka 2023 kwa madai ya usalama wa taifa hatua iliyodaiwa kuiathiri biashara ya Micron nchini China.
Ziara hiyo inatajwa kuwakutanisha viongozi wa sekta mbalimbali zikiwemo teknolojia, benki, usafiri wa anga, biashara ya chakula, pamoja na mitandao ya kijamii, huku ikionyesha namna biashara kubwa za Marekani zinavyoendelea kutegemea soko la China licha ya mvutano wa kisiasa na kiuchumi uliopo kati ya nchi hizo mbili.