
Yanga imepoteza mchezo wao wa kwanza msimu huu baada ya kupokea kichapo cha mabao 3-2 dhidi ya Dodoma Jiji FC katika mchezo uliokuwa na ushindani mkubwa uliofanyika kwenye uwanja wa Dodoma.
Licha ya kupoteza mchezo huo, Yanga bado wanaendelea kusalia kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya NBC wakiwa na pointi 54 baada ya kucheza mechi 23, wakiwa mbele ya watani wao Simba kwa tofauti ya pointi tano, huku Simba wakiwa na mchezo mmoja mkononi.
Katika mchezo huo, Yanga walitangulia kupata mabao mawili kupitia nyota wao Okello katika dakika ya 2 na 42, hali iliyowapa matumaini ya kuondoka na ushindi.
Hata hivyo, Dodoma Jiji walipata bao la kujifunga kupitia Mwamnyeto dakika ya 28, kabla ya kurejea kwa nguvu kipindi cha pili na kusawazisha kupitia David Kibuta dakika ya 90, kisha Waziri Junior kufunga bao la ushindi dakika ya 90+5 na kuipa Dodoma Jiji pointi tatu muhimu.
Matokeo hayo yamekuwa pigo kwa Yanga kwa kuwa ni mara yao ya kwanza kupoteza mchezo msimu huu, lakini bado wanaendelea kuongoza ligi katika mbio za ubingwa.