
Wakazi wa Kijiji cha Mungushi, Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, sasa wameondokana na changamoto za muda mrefu za mawasiliano baada ya uzinduzi wa mnara mpya wa Airtel 4G.
Miundombinu hii ya Airtel Tanzania imeimarisha huduma za intaneti ya kasi na mawasiliano katika Kijiji cha Mungushi na maeneo ya jirani kama Gezaulole, Bomani, Mboni na Uzunguni.
Vijiji hivi sasa vinapata huduma za kidigitali na kufanya miamala ya fedha kwa njia ya simu kwa uhakika na rahisi.
Akizungumza wakati wa uzinduzi, Mwenyekiti wa Kijiji cha Mungushi, Lameck Simbo, alisema kwa muda mrefu wananchi walikumbwa na tatizo la mtandao hafifu, hali iliyokuwa ikiathiri mawasiliano na huduma za kifedha kwa simu.
Alisema huduma ya 4G sasa itaimarisha shughuli za kiuchumi ikiwemo kilimo, ufugaji, biashara na utalii katika maeneo ya hifadhi ya Mlima Kilimanjaro na wilaya jirani.
“Awali tulikuwa na changamoto za mawasiliano, hasa maeneo kama Matnonda. Sasa Airtel imeboresha sana huduma. Tofauti na baadhi ya mitandao mingine, Airtel hapa ni ya kuaminika zaidi,” alisema Simbo.
Aliongeza kuwa mawasiliano bora ni msingi muhimu wa ukuaji wa uchumi, kwani huwezesha biashara kufanyika kwa ufanisi na haraka zaidi.
“Kila biashara inategemea mawasiliano. Yanapokuwa bora, uchumi hukua kwa sababu watu hufanya kazi kwa ufanisi zaidi,” alisema.
Simbo pia aliishukuru Airtel kwa kuunga mkono juhudi za maendeleo za Serikali ya Tanzania chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kupitia uwekezaji wa miundombinu ya kidigitali.
Meneja wa Biashara wa Airtel Kanda ya Kilimanjaro, Faustin Mtui, alisema uwekezaji katika mtandao wa 4G vijijini unalenga kupunguza pengo la kidigitali na kuongeza fursa kwa wananchi.
“Leo tunazindua rasmi huduma bora za Airtel 4G katika eneo hili. Mnara huu utahudumia Mfungushi, Gezaulole, Bomani, Mboni na Uzunguni,” alisema Mtui.
Alisema huduma hiyo itaboresha mawasiliano, shughuli za biashara na upatikanaji wa huduma za kifedha kupitia simu.
Pia aliwahimiza vijana kutumia fursa zinazotokana na upatikanaji wa intaneti ya kasi kujiajiri.
“Hii ni fursa kwa vijana kujiajiri. Wanaweza kufanya kazi kama mawakala wa Airtel Money, usajili wa SIM kadi, na biashara ya vifurushi vya intaneti, ruta na huduma nyingine za mawasiliano,” alisema.
Mtui alisema uwekezaji huo unachangia kupunguza changamoto ya ajira kwa kutoa fursa za moja kwa moja ndani ya jamii.
Mkazi wa Mungushi, Kophi Mbude, alisema hapo awali walikumbwa na changamoto kubwa za mawasiliano na kulazimika kusafiri umbali mrefu kupata huduma.
“Tunaishukuru sana Airtel kwa mnara huu. Kabla ya huduma hii, tulikuwa na changamoto kubwa ya mawasiliano na huduma za fedha kwa simu,” alisema.
Alisema sasa huduma za Airtel 4G zimeimarisha miamala na biashara za kila siku kwa urahisi zaidi.
Mnara huu unatarajiwa kuongeza ushirikishwaji wa kidigitali, kuimarisha biashara za ndani na kukuza ustahimilivu wa kiuchumi katika jamii za eneo la Mlima Kilimanjaro.