
Kiongozi Mstaafu wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe, ameikosoa vikali Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kufuatia taarifa zinazodaiwa kuhusisha hatua za kutaka kukifuta Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), akisema kuwa hatua yoyote dhidi ya chama hicho ni tishio kwa demokrasia nchini.
Kupitia andiko lake alilochapisha Mei 14, 2026 katika mtandao wa X, Zitto alisema zama za Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kuwa “mchezaji namba 12 wa CCM” zimekwisha na kuitaka dola kusoma alama za nyakati.
“Msajili stop this nonsense ya kutaka kufuta Chadema, utafutwa wewe, no doubt about this,” aliandika Zitto.
Mwanasiasa huyo alisema Tume ya Chande iliyoundwa na Rais ilibaini kuwa wananchi wana malalamiko kuhusu Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kwa kile alichodai kuwa ni kutotenda haki katika usimamizi wa shughuli za vyama vya siasa.
Alidai kuwa badala ya ofisi hiyo kujirekebisha, imeendelea kurudia makosa ambayo amesema yalichangia migogoro ya kisiasa na matukio ya vurugu yaliyoanza Oktoba 29.
Zitto pia alisema kuna madai ya kuwepo kwa ukiukwaji unaofanywa na CCM ambao haujachukuliwa hatua na Msajili wa Vyama vya Siasa, huku akisisitiza kuwa Watanzania wanaelewa kinachoendelea kisiasa nchini.
“Watanzania sio mabwege, tunachukulia tishio lolote dhidi ya Chadema ni tishio dhidi ya demokrasia,” alisema.
Aidha, aliitaka Serikali pamoja na vyombo vya usalama kuviacha vyama vya siasa vifanye shughuli zake kwa uhuru bila kuingiliwa, akisema siasa za ushindani zinapaswa kuachiwa vyama vyenyewe.
Kauli hiyo imekuja baada ya Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika kusema kwamba licha kufunguliwa na mahakama kuu kufanya siasa, ofisi ya msajili wa vyama imewaandikia barua kuwataka wajieleze kuhusu mambo mbalimbali kuhusu chama chao, jambo ambalo Mnyika amesema ni jitihada za ofisi hiyo kudhoofisha chama chake..