
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeeleza taarifa mpya kuhusu msaidizi wa mwenyekiti wake, Tundu Lissu, David Jumbe, kufuatia madai mbalimbali yaliyoenea kuhusu tukio lake la kukamatwa na kupatikana akiwa na pingu mikononi.
Akizungumza na waandishi wa habari, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Bara), Amani Golugwa amesema taarifa alizozipata kutoka kwa mke wa Jumbe zinaeleza kuwa mumewe amerejea nyumbani akiwa bado na pingu hizo.
Golugwa amesema mapema leo Alhamisi, Mei 21, 2026, maafisa wa Jeshi la Polisi kutoka Kituo cha Oysterbay walifika katika makao makuu ya Chadema wakieleza kuwa wanamtafuta Jumbe, wakidai alitoweka akiwa na pingu.
Kwa mujibu wa Chadema, polisi hao pia walieleza kuwa huenda Jumbe alijificha ndani ya ofisi za chama hicho, hali iliyosababisha ombi la kuruhusiwa kumtafuta.

Hata hivyo, Golugwa alisisitiza kuwa Jumbe tayari alikuwapo nyumbani kwake na akaomba polisi kwenda kumfungua pingu badala ya kuendelea na msako.
“Tunawaambia Polisi Jumbe yupo nyumbani kwake, waende wakamfungulie pingu,” alisema Golugwa.
Awali, taarifa zilizosambaa mitandaoni zilidai kuwa Jumbe alichukuliwa nyumbani kwake eneo la Mabwepande, Bunju jijini Dar es Salaam usiku wa kuamkia leo na watu wasiojulikana waliomuingiza kwenye gari na kuondoka kwa kasi, huku akidaiwa kupoteza kiatu wakati wa tukio hilo.
Hata hivyo, baadaye Jeshi la Polisi Kituo cha Oysterbay lilieleza kuwa David Jumbe alifikishwa kituoni hapo kwa ajili ya mahojiano. Polisi hao pia walimfungua pingu zilizokuwa zimembana mkononi kwa muda na kusababisha uvimbe.
Jeshi la Polisi katika Kanda Maalum ya Dar es Salaam bado halijatoa taarifa rasmi ya kina kuhusu tukio hilo.
