
Mohamed Salah ameweka historia ya hisia kali baada ya kuaga rasmi klabu ya Liverpool F.C. katika mechi yake ya mwisho iliyomalizika kwa sare ya 1-1 dhidi ya Brentford F.C. katika Uwanja wa Anfield.
Salah alishuhudia shangwe kubwa kutoka kwa mashabiki baada ya kubadilishwa dakika ya 74, akipokelewa na standing ovation na baadaye kupita kwenye gwaride la heshima kutoka kwa wachezaji na benchi la ufundi la Liverpool huku akiwa ameguswa na hisia kali.
Nyota huyo wa Misri amesema alilia zaidi kuliko alivyowahi kulia maishani mwake, akieleza jinsi ilivyokuwa vigumu kuondoka katika klabu aliyochezea kwa miaka tisa na kuisaidia kushinda mataji makubwa.
Katika kipindi chake Liverpool, Salah amecheza mechi 442, akifunga mabao 257 na kutoa asisti 120, huku akivunja rekodi mbalimbali ikiwemo kuwa mfungaji bora wa muda wote wa klabu hiyo kwenye Premier League.
Pia amevunja rekodi ya asisti kwa Liverpool iliyokuwa ikishikiliwa na Steven Gerrard, na kuacha historia kubwa ndani ya klabu hiyo.
Salah anaondoka akiwa miongoni mwa wachezaji walioacha alama kubwa zaidi Anfield, akishinda mataji ya ligi, Ligi ya Mabingwa na tuzo kadhaa za mfungaji bora katika kipindi chake cha mafanikio makubwa.