×

Wanafunzi 16 Wafariki, 74 Wajeruhiwa Katika Ajali Ya Moto Shuleni Kenya

WANAFUNZI 16 wamefariki dunia huku wengine 74 wakijeruhiwa baada ya moto mkubwa kuteketeza bweni la wanafunzi katika Chuo cha Wasichana cha Utumishi kilichopo Gilgil, Kaunti ya Nakuru nchini Kenya, usiku wa kuamkia leo Alhamisi Mei 28, 2026.

Kwa mujibu wa taarifa za polisi, moto huo ulizuka majira ya saa saba usiku na kuteketeza bweni la Meline Waithera lililokuwa na zaidi ya wanafunzi 220 wa Kidato cha Pili hadi cha Nne. Timu za uokoaji zikiwemo wazima moto, polisi pamoja na wahudumu wa dharura zilifika eneo la tukio kuanza oparesheni ya uokoaji na kuwahesabu wanafunzi waliokuwepo.

Maafisa wa polisi wamesema wanafunzi wengi waliopona walijeruhiwa wakati wakijaribu kukimbia kujiokoa huku baadhi wakilazimika kuruka kutoka ghorofa za juu kutokana na moto huo kusambaa kwa kasi.

Naibu Mkuu wa Pili wa Jeshi la Polisi nchini Kenya, Masoud Mwinyi amesema uchunguzi umeanza rasmi ili kubaini chanzo cha moto huo huku akiwataka wananchi kuepuka kusambaza taarifa zisizothibitishwa.

“Timu za DCI na wataalamu wa uchunguzi wa kisayansi tayari zipo eneo la tukio na uchunguzi unaendelea,” amesema Mwinyi.

Ameongeza kuwa baadhi ya wanafunzi walikimbia kuelekea maeneo ya jirani kutokana na taharuki kubwa iliyotokea usiku huo na kwamba zoezi la kuwatafuta na kufanya uhakiki wa majina linaendelea.

Wazazi walijaa nje ya geti la shule tangu alfajiri wakitafuta taarifa za watoto wao huku hali ya huzuni na hofu ikitawala eneo hilo. Uongozi wa shule ulisema wazazi pekee ndio watakaoruhusiwa kuingia ndani kusaidia katika zoezi la utambuzi wa wanafunzi.

Mashuhuda wa tukio hilo wamesema kulikuwa na mayowe na taharuki kubwa wakati wanafunzi wakijaribu kujiokoa kutoka katika jengo lililokuwa likiwaka moto.

Mmoja wa ndugu wa wanafunzi, Wambui Nderitu amesema alipokea simu usiku akiarifiwa kuhusu moto huo na alipofika shuleni alikuta hali ya sintofahamu huku taarifa za vifo na majeruhi zikisambaa.

“Nilikuta wazazi wengi wakiwa na hofu kubwa. Tulielekezwa kupanga foleni huku tukisubiri taarifa za watoto wetu,” amesema.

Nderitu amesema mpwa wake amenusurika lakini amevunjika mguu baada ya kujeruhiwa wakati wa kujiokoa.

Chanzo cha moto huo bado hakijajulikana huku mamlaka zikiahidi kutoa taarifa zaidi baada ya uchunguzi kukamilika na wanafunzi wote kuthibitishwa.

BARUA 25 za RAIS! AFICHUA KUFIKA HADI kwa PAPA LEO – “TUMEDANGANYWA TAARIFA SIYO ALIZOANDIKA RAIS”..

Leave a Comment