
Mvutano kati ya Marekani na Iran umeendelea kushika kasi baada ya ripoti kueleza kuwa Rais Donald Trump ametuma pendekezo jipya lenye masharti magumu zaidi kuhusu makubaliano ya amani na mpango wa nyuklia wa Tehran.
Mjadala huo umeibuka huku mkuu wa mazungumzo wa Iran, Mohammad Bagher Qalibaf, akisisitiza kuwa taifa hilo halitakubali makubaliano yoyote ambayo hayatalinda kikamilifu haki za wananchi wa Iran.
Kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari vya Marekani, pendekezo hilo jipya linaweza kuchelewesha zaidi makubaliano ya kumaliza rasmi vita vya Mashariki ya Kati na kufunguliwa tena kwa njia muhimu ya biashara ya mafuta kupitia Mlango Bahari wa Hormuz.

Trump amesema kipaumbele chake ni kuhakikisha Iran haitengenezi silaha za nyuklia na pia kurejesha usalama wa njia hiyo ya kimataifa ya usafirishaji wa mafuta. Hata hivyo, Iran imeendelea kupinga baadhi ya madai ya Marekani, ikisema bado kuna tofauti kubwa kwenye masuala muhimu ya mazungumzo.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, amesema taarifa nyingi zinazoendelea kutolewa ni tetesi hadi pale makubaliano rasmi yatakapofikiwa.
Iran pia imeweka sharti la kuachiwa dola bilioni 12 (TSh trilioni 31.2) za mali zake zilizoshikiliwa kabla ya kuingia kwenye mazungumzo ya kina kuhusu mpango wake wa nyuklia.

Wakati huo huo, hali ya usalama imeendelea kuwa tete baada ya Iran kudai kuidungua droni ya kijeshi ya Marekani iliyokuwa karibu kuingia kwenye anga yake. Ripoti nyingine zimeonyesha kuwa Iran imeanza kurejesha baadhi ya miundombinu yake ya makombora iliyoharibiwa katika mashambulizi ya awali ya Marekani na Israel.
Katika upande mwingine, mgogoro wa Lebanon nao umeendelea kuathiri mazungumzo hayo, huku mapigano kati ya Israel na kundi la Hezbollah yakiendelea licha ya kuwepo kwa makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyowahi kutangazwa mwezi Aprili.