
Kupitia akaunti yake ya Instagram, Mbunge wa Buchosa, Eric Shigongo, ameandika ujumbe mzito akizungumzia changamoto katika utekelezaji wa Sheria ya Manunuzi nchini.
Katika ujumbe wake, Shigongo amesema kuwa bado kuna mapungufu katika utekelezaji wa sheria hiyo licha ya juhudi za maboresho yaliyofanyika kupitia bajeti iliyopita, ambapo ilipitishwa kwamba miradi yote yenye thamani ya chini ya shilingi bilioni 50 ifanywe na wazawa ili kuwalinda Watanzania katika sekta ya biashara na ajira.
Ameeleza kushangazwa na hali inayoendelea, akidai kuwa bado baadhi ya kampuni za kigeni, hususan zile za Kichina, zinaendelea kupata zabuni za miradi yenye thamani ndogo kama shilingi bilioni 5. Amesema hali hiyo inahitaji ufafanuzi wa kina ili kubainisha wazi kampuni za ndani na zile za nje, ili kuondoa mianya ya baadhi ya wawekezaji wa kigeni kutumia Watanzania kama mbele (front) huku wao wakinufaika moja kwa moja na miradi hiyo.
Shigongo amesisitiza kuwa ni muhimu kwa Serikali na mamlaka husika kuhakikisha Watanzania wananufaika ipasavyo na rasilimali na fursa za kiuchumi zilizopo nchini, badala ya kushuhudia wageni wakichukua nafasi zinazopaswa kunufaisha wazawa.
Ujumbe wake umeibua mjadala mpana mitandaoni kuhusu utekelezaji wa sheria za manunuzi na ushiriki wa wazawa katika miradi ya maendeleo.
