
MKAZI WA CHUNYA, Bi Agnes Obeid Ole amelia machozi ya furaha mbele ya Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba baada ya kusikilizwa kero yake na kutolewa uamuzi kwamba mdaiwa atafutwe na amlipe sh. milioni 181 anazozidai.
“Kamanda wa Polisi mtafute huyo bwana. Mahakama ilikwishatoa hukumu na ikampa mama ushindi. Asakwe popote alipo, arudishe vifaa na arudishe fedha za huyu mama,” amesema Waziri Mkuu na kuamsha shangwe kwa wananchi waliokuwepo.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumamosi, Juni 6, 2026) wakati akizungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya soko la Ifunda, wilayani Iringa, mkoani Iringa.

Akielezea kero yake, Bi. Agnes alisema kuwa kabla mumewe hajafariki, walikuwa wanachimba dhahabu kwenye mgodi wao huko Chunya lakini walimuomba rafiki yao, Bw. Lelevasi Fishulo mwenye mashine za kuchenjua washirikiane naye ili baadaye wagawane naye faida.
“Tulipata sh. milioni 362 lakini akasema amepata dharura na akaomba atulipe baadaye. Tukamkubalia. Mgao wetu ulikuwa sh. milioni 181 lakini siku ya kulipwa mume wangu akafariki, kwa hiyo nikaacha kufuatilia sababu ya maombolezo.”

Bi. Agnes anasema baada ya mwaka mmoja kupita akamfuata kudai hela yake lakini hakumpa. “Nikaenda Serikali ya kijiji akaitwa kwa miezi mitatu hakutokea, nikaenda polisi akaitwa lakini ikapita miezi minne hakutokea ndipo nikaenda mahakamani kwa masuala ya mirathi,” amesema.
Amesema alifungua kesi ya madai ya kudhulumiwa mali baada ya mumewe kufariki na mahakama ikampa haki ya kuwa msimamizi wa mirathi.